KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MAKAZI YA MSOMERA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imeridhishwa na namna Serikali ilivyowajali wananchi waliohamia Kijiji cha Msomera kwa hiyari yao wenyewe ili kupisha shughuli za uhifadhi katika eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kufuatia serikali kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya kutolea huduma za kijamii.
Akizungumza baada ya kutembelea Kijiji Cha Msomera, Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe Ally Makoa ( MB), licha ya kutoa pongezi hizo amesema Kamati yake imeshuhudia mambo makubwa yaliyotekelezwa na Serikali ndani ya muda mfupi ili kuwafanya wakazi waliohamia kwa hiyari katika kijiji hicho wawe na maisha bora zaidi.
"Leo tumejionea wenyewe majengo bora kabisa ya madarasa na vifaa vya kisasa vya kufundishia na Mazingira yake, nyumba nzuri, maji ya kutosha, majosho mazuri ya wanyama, Barabara inayopitika vizuri, hakika Wizara ya Maliasili na Serikali kwa ujumla mnahitaji Pongezi sana". Amesisitiza.
Mhe. Makoa ameongeza kuwa Kamati yake imefarijika sana na kauli za wakazi wa Kijiji hicho kwamba maisha yao kwa sasa ni bora zaidi kuliko walikotoka na zaidi wamepata fursa za kilimo na biashara mbalimbali zikiwemo za usafirishaji abiria na bidhaa, maduka, vyakula, Ufugaji wa Kisasa na kilimo
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana amemshukuru Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson kwa kuridhia Kamati hiyo iende Kijiji cha Msomera kuona kazi nzuri inayoendelea kufanywa na Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuboresha maisha ya Watanzania
Waziri Balozi Dkt. Chana ameongeza kuwa Wizara anayoiongoza itanaendea kushirikiana kikamilifu na Wizara zingine katika kuhakikisha mazingira ya Kijiji cha Msomera kinazidi kuwa rafiki kwa wakazi wake na kwa wote wanaoendelea kuhamia kwa hiyari yao.
Aidha, Mhe.Balozi Dkt.Chana ameendelea kutoa rai kwa wote wanaopotosha umma kuhusu zoezi la wananchi wanaohama kwa hiyari yao kutoka Hifadhi ya Taifa Ngorongoro na kuhamia Mosomera Tanga au maeneo mengine waache mara Moja kupotosha jamii.
KAMATI YA BUNGE YARIDHISHWA NA MAKAZI YA MSOMERA
Reviewed by Fahadi Msuya
on
September 03, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
September 03, 2022
Rating:





Post a Comment