Header AD

header ads

KILINDI YAJA KWA KASI YAJIPANGA KUFANYA VIZURI KATIKA ELIMU

 


Na Hadija Bagasha Kilindi, 

Halmashauri ya wilaya ya kilindi imesema pamoja na jitihada zinazofanywa na serikali za kuboresha sekta ya elimu Halmashauri ya wilaya hiyo imeamua kusaidia watoto wenye uwezo wa kitaaluma wanaotoka mazingira magumu ili kuwaendeleza kitaaluma kupitia uanzishwaji wa mfuko wa maendeleo ya elimu. 

Mfuko huo piautasaidia kulipa posho walimu wasioajiriwa wanaojitolea kufundisha shule za msingi na sekondari ili kukabili upungufu wa walimu wilayani humo. 


Kauli hiyo imetolewa na afisa elimu msingi wa wilaya hiyo Danstan Ntauka wakati  akisoma taarifa ya mfuko huo kwenye kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya wilaya ya Kilindi kikao kilichoambatana na uzinduzi wa vitabu vya muongozo wa elimu sambamba na uanzishwaji wa mfuko wa maendeleo ya elimu Kilindi. 


Afisa elimu huyo amesema jambo jingine ambalo mfuko huo utajihusisha nalo ni kusaidia serikali kuweka msawazo wa walimu ili kuimarisha timu ya ufundishaji katika shule za msingi na sekondari. 

Alisema mfuko huo utalipa stahiki za uhamisho na kusaidia serikali kununua mafuta ya kuhamisha walimu sambamba na kurekebisha uharibifu wa chombo cha usafiri uliotokea wakati wa kuhamisha walimu. 

Awali akizungumzia mfuko huo afisa elimu huyo amesema uanzishwaji wa mfuko huo umezingatia changamoto mbalimbali zinazojitokeza katika uanzishwaji wa elimu licha ya kwamba serikali imekuwa ikiwekeza kwa kiasi kikubwa ili kufanikisha maendeleo ambayo Taifa limekusudia katika sekta hiyo ya elimu. 


"Pamoja na jitihada hizo zote bado maeneo mengi yanahitaji usaidizi yana changamoto nyingi kwahiyo Halmashauri ya wilaya ya kilindi kwa pamoja imeweka jitihada za makusudi ili kuiunga mkono serikali katika kutatua changamoto hizo kwa kuunganisha nguvu za wananchi wote ili kuchangia jitihada hizo katika kuboresha elimu katika Halmadhauri yetu, "alisistiza Ntauka. 

Alisema uwepo wa mfuko huo wa maendeleo ya elimu katika wilaya hiyo ni jitihada za Halmashauri hiyo kwa msingi wa kutatua changamoto mbalimbali katika sekta hiyo. 

"Mfuko huu sio wa kibiashara bali uko kwajili ya kutimiza malengo yakiwemo kuhamasisha na kuboresha maendeleo ya elimu ya awali,  msingi,  sekondari na ufundi stadi ndani ya Halmashauri ya wilaya ya kilindi,  kujenga madarasa,  nyimba za walimu hosteli za wanafunzi maabara,  vyoo na kutengeneza samani za shule za msingi,  sekondari na vituo vya ufundi stadi, "alisema Ntauka

Awali akizungumza katika kikao hicho mara baada ya kuzindua vitabu vya muongozo wa elimu wilayani humo,  Mkuu wa wilaya hiyo Abel Busalama amesema katika awamu ya Rais Samia Suluhu Hassan changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiikabili wilaya hiyo zimepatiwa ufumbuzi. 


"Katika utawala wa mwaka mmoja wa Rais wetu mpendwa mheshimiwa Samia Suluhu changamoto nyingi ambazo zilikuwa zikiikabili wilaya hii zimeweza kufanyiwa kazi kwenye masuala ya utawala tumeona jinsi Halmashauri yetu na ofisi mbalimbali za serikali wilayani kwetu zimeweza kuongezewa watumishi lakini pia tumepata majengo mbalimbali ya kiutawala ikiwemo mahakama ya wilaya, "alisema Busalama.

Aidha alisema kwa upande wa uzalishaji sekta karibuni zote zimeguswa ikiwemo sekta ya kilimo ambapo Rais amekuja na suala la ruzuku ya pembejeo hivyo amewataka madiwani kuchangamkia fursa hiyo ili kujikwamua kiuchumi. 

Akizungumzia sekta ya elimu Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa wilaya hiyo imeendelea kujipanga na kuhakikisha inafanya vizuri katika matokeo yake na kuhakikisha hairudi nyuma kitaaluma huku akiipongeza shule ya Mkindi Sekondari iliyopo wilayani humo kwa kufanya vizuri katika matokeo yake ya kidato cha sita na kushika nafasi ya 9 kitaifa jambo ambalo wilaya hiyo imejivunia. 

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Gracian Makota amewataka madiwani wa Halmashauri hiyo kwenda kusimamia vyema suala la usafi katika maeneo yao kila siku ya jumamosi ya mwisho wa mwezi. 


"Kila jumamosi ya mwisho wa mwezi itakuwa ni siku ya usafi kwenye maeneo yetu tunawaomba sana sana waheshimiwa mafiwani kwa sasa hili limeshakuwa ni agizo la kisheria twende tukalisimamie ufanywaji wake wa kazi katika maeneo yetu wananchi wajitokeze kufanya usafi kwenye maeneo yao, "alibainisha Makota. 

Naye Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Idrisa Mgaza amesema wao kama viongozi wa wilaya hiyo watakwenda kuwasaidia wanafunzi hao waliofanya vizuri katika shule hiyo ya Mkindi na shule nyingine ili wasikwame kwajili ya hali ngumu za familia zao. 

Uzinduzi wa muongozo wa elimu Kilindi umefanywa na Mkuu wa wilaya hiyo pamoja na uzinduzi rasmi wa mfuko wa maendeleo ya elimu Kilindi ulioambatana na sherehe za kupongeza Mkindi sekondari kwa matokeo mazuri ya mtihani wa kidato cha sita 2022 kiasi cha kushika nafasi ya 9 kitaifa ambayo imetangaza vyema wilaya ya kilindi na Mkoa kwa ujumla. 


KILINDI YAJA KWA KASI YAJIPANGA KUFANYA VIZURI KATIKA ELIMU KILINDI YAJA KWA KASI YAJIPANGA KUFANYA VIZURI KATIKA   ELIMU Reviewed by Fahadi Msuya on September 26, 2022 Rating: 5