Header AD

header ads

MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA NI TATIZO KATIKA MKOA WA TANGA



Na Hadija Bagasha Tanga, 

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Omary Mgumba amesema matumizi ya dawa za kulevya bado ni tatizo katika Mkoa wa Tanga jambo ambalo linahatarisha usalama wa wananchi. 

Mgumba amesema hali ya ulinzi na usalama katika Mkoa wa Tanga bado ni tatizo ambalo linahitaji kila mwanajamii kuona namna tatizo hilo litakavyokwisha. 


Mgumba ametoa kauli hiyo wakati akiwa kwenye kikao maalumu cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya jiji hilo cha kujitambulisha ikiwa ni muendelezo wa vikao vyake anavyovifanya na madiwani vya kujitambulisha mara baada ya kuhamishiwa Mkoani Tanga. 

Mgumba ameyataja maeneo matatu ambayo bado yanahitaji kuangaliwa kwa jicho la kipekee huku akitaja kushamiri kwa matumizi ya dawa za kulevya kwenye baadhi ya maeneo Mkoani humo na hivyo kuhatarisha usalama wa jamii. 

Mgumba amesema baadhi ya maeneo yanauza dawa za kulevya na jamii inaona jambo hilo ni la kawaida badala ya kushirikiana na vyombo vya dola kupambana na vitendo hivyo ambavyo vikiachwa vinaathiri nguvu kazi ya Taifa.


"Dawa za kulevya zinauzwa hadharani kwenye maeneo yetu  na sisi tunayafumbia macho jambo hili halipaswi kabisa kuvumiliwa linatuharibia nguvu kazi yetu ya Taifa tunapaswa kulipiga vita na kupambana nalo, "alisisitiza Mgumba. 

Eneo lingine linalohatarisha hali ya ulinzi na usalama wa Mkoa huo ni pamoja na biashara ya usafirishaji wa binadamu ambayo inafanywa na jamii ya eneo husika kusaidia wageni kupita kwenye mipaka ya nchi kama vile Horohoro bila kufahamu madhara yake kwa Taifa,  jambo ambalo amesema kwenye uingozi wake anataka vitu hivyo vikome mara moja. 

Tishio lingine alilolitaja ni usalama wa chakula ambapo kwa tafiti iliyofanywa na serikali kupitia wizara ya kilimo  hali ya usalama wa chakula katika Mkoa wa Tanga hususani katika wilaya mbili za Mkinga na Handeni sio nzuri jambo ambalo amesema limekuwa hata na madhara kwa wanafunzi wanaosoma kwenye shule za msingi na sekondari. 

Akiwa katika kikao hicho Mgumba amelipongeza Jiji la Tanga kwa kufanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato na kuongoza majiji mengine hapa nchini katika mwaka wa fedha 2021/2022 kwa kukusanya mapato kwa asilimia 113 ya lengo la mwaka.

Awali, akiwasilisha taarifa ya Jiji la Tanga kwa Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi wa Jiji hilo Sipora Liana amesema kwa mwaka wa fedha 2021/2022 unaoishia mwezi Juni 2022, Halmashauri imefanikiwa kupeleka katika miradi mbalimbali ya maendeleo zaidi ya shillingi billion 6.6 ikiwa ni katika utekelezaji wa utoaji wa asilimia 60 ya mapato ya ndani.

"Kati ya fedha hizi, shillingi 1.1 billion zimeelekezwa katika sekta ya afya, shillingi 2.7 billion sekta ya elimu, shillingi 167 million zimepelekwa eneo la utawala katika ujenzi wa ofisi za kata, na utoaji wa mikopo ya wanawake, vijana na wenye ulemavu ni 1.1 billion, sekta ya biashara ikitengewa million 100 kwa ajili ya ujenzi wa soko, shillingi 410 million zikitumika katika shughuli za anwani za majazi, na miradi mingine ya uwekezaji na ufuatiliaji ikigharimu shillingi 995 million". Amebainisha Liana.

Hata hivyo Mgumba amesema yupo tayari kuanza kazi baada ya kuhitimisha ziara ya kujitambulisha kwa Wilaya na Halmashauri za mkoa wa Tanga.


MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA NI TATIZO KATIKA MKOA WA TANGA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA NI TATIZO KATIKA MKOA WA TANGA Reviewed by Fahadi Msuya on September 09, 2022 Rating: 5