SERIKALI YAHIMIZA UFUGAJI WA NYUKI NA UZALISHAJI WA ASALI NCHINI
Serikali imetoa wito kwa wananchi waendelee kuchangamkia fursa ya ufugaji wa nyuki kutokana na uwepo wa mahitaji makubwa ya asali ndani na nje ya nchi.
Aidha, imesema Tanzania ina uwezo wa kuzalisha tani 138,000 za asali na kuongeza kuwa kwa sasa takribani tani 31,672 zinazalishwa kiwango ambacho ni sawa na asilimia 22 ya uzalishaji.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Maliasili na utalii Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana alipokuwa akizindua Kamati ya Kitaifa ya Ushauri ya Ufuatiliaji ya Ufugaji nyuki (NABAC) ambapo ameitaka kamati hiyo kuangalia kwa kina eneo hilo ili itoe ushauri kwa Serikali kuongeza kiwango cha uzalishaji wa asali hapa nchini.
‘’Katika kufanikisha jambo hili natoa rai kwa taasisi zetu zifanye kazi kwa karibu zaidi na wafugaji nyuki hasa wale wanaoishi jirani na maeneo ya hifadhi ili waweze kufunga nyuki katika maeneo hayo kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizopo pamoja na kuwapa msaada na ushauri wa kitaalam wa maeneo bora ya kutekeleza adhma hii muhimu kwa uchumi wa nchi yetu”
Waziri Pindi Chana ameongeza kuwa ufugaji nyuki ni moja ya nyezo muhimu katika utunzaji wa mazingira na hutumika kama njia ya kuzuia wanyamapori waharibifu hususan tembo kuingia kwenye mashamba na makazi ya wananchi huku akitoa wito kwa wataalam wa Idara ya Misitu na Nyuki waongeze nguvu katika utoaji wa elimu kuhusu ufugaji nyuki kwa makundi ya vijana na wanawake katika Halmashauri mbalimbali hapa nchini.
“ Naomba muongeze nguvu kwenye programu za utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu ufugaji nyuki mkianza na maeneo ya jiji la Dodoma ambapo ni makao makuu ya nchi, anzisheni utaratibu wa kuwafikia vijana na makundi ya kina mama kwenye Halmashauri ili wanufaike na fursa hii ya ajira kwa kuanzisha shamba darasa ambalo litatumika kama mfano katika ufugaji nyuki” Amesisitiza Balozi Dkt. Pindi Chana.
Kuhusu Kamati hiyo ya Kitaifa aliyoizindua Balozi Dkt. Pindi Chana ameitaka izifanyie kazi changamoto mbalimbali pamoja na kutoa ushauri kwa Serikali juu ya namna bora ya kuwezesha upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kufugia nyuki,kuchakata na kuhifadhi mazao ya nyuki kwa gharama nafuu hapa hapa nchini badala ya kuagiza kutoka nje.
“Kamati hii itushauri namna gani tunaweza kuongeza uzalishaji wa asali angalau kufikia asilimia 50 ya uwezo wa uzalishaji uliopo pia ishauri kuhusu utaratibu gani unaweza kutumiwa na Serikali pamoja na wadau wengine wakati wa kuwezesha wadau mbalimbali kwenye sekta ya ufugaji nyuki mfano watu binafsi,vikudni,vyama vya ushirika ili kuleta ufanisi na tija.’’Amesisitiza.
Mbali na hilo ameitaka Kamati hiyo kushauri namna bora ya kukabiliana na uharibifu wa maeneo yanayofaa kwa ajili ya shughuli ya ufugaji nyuki hapa nchini ‘’Kamati hii pia ishauri namna bora ya kuimarisha Utalii wa Nyuki kwa lengo la kuhakikisha kuwa sekta hii inachangia katika ukuaji wa shughuli za asili hapa nchini.’’
SERIKALI YAHIMIZA UFUGAJI WA NYUKI NA UZALISHAJI WA ASALI NCHINI
Reviewed by Fahadi Msuya
on
September 20, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
September 20, 2022
Rating:




Post a Comment