Breaking news- Serengeti Girls yawaahidi watanzania ushindi
Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa ameitakia kila la kheri timu ya Serengeti Girls katika mashindano ya Kombe la Dunia yanayoanza leo nchini India huku ikitarajia kutupa karata yake ya kwanza majira ya saa 11:30 jioni leo dhidi ya timu ya Japan, huku timu hiyo ikiwaahidi watanzania ushindi.
Akiongea leo muda mfupi kabla ya kuanza mechi hii, Mhe. Mchengerwa amesema Mhe. Rais na watanzania wanafuatilia kwa karibu na wanamatumaini makubwa na timu hiyo na kuwataka kucheza kufa na kupona ili kurejesha kombe hilo nyumbani.
"Mimi kama Waziri sitarajii kusikia kuwa mmetolewa, ninachotaka kusikia ni nyie kurudi na kombe nyumbani. Mhe Rais ana matarajio makubwa " amesisitiza, Mhe. Mchengerwa
Amefafanua kuwa Serikali inatumaini kuwa timu hiyo inakwenda kufanya vizuri zaidi kuliko timu ya Soka ya Taifa ya wenye ulemavu (Tembo Warriors) iliyofuzu kuingia robo fainali na kuiletea Tanzania heshima kubwa.
Aidha, amewataka wachezaji kuonesha viwango vya juu katika mashindano haya ili waweze kununuliwa na vilabu vikubwa duniani.
Pia Mhe. Waziri amewataka viongozi walioambatana na timu hiyo kusimamia kikamilifu jukumu walilopewa na taifa na kuhakikisha kuwa timu inakuwa na hamasa kubwa na inashinda.
Amesema dhamira Serikali kwa sasa ni kuibua vipaji vya vijana na kuwaomba watanzania kuiombea timu hii ili ushinde.
Nahodha wa timu hiyo Noela Luhala amemhakikishia Mhe. Waziri Mchengerwa kuwa timu yake inakwenda kupambana kufa na kupona kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mashindano ili kulinda heshima ya Rais na watanzania hatimaye kurejesha kombe nchini.
Breaking news- Serengeti Girls yawaahidi watanzania ushindi
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 12, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 12, 2022
Rating:


Post a Comment