MAHMOUD AIBUKA MSHINDI MWENYEKITI MPYA CCM WILAYA PANGANI
Na Hadija Bagasha Pangani,
Aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM Wilaya ya Pangani Rajab Abdulrahman amemtwisha mzigo Mwenyekiti mpya wa Wilaya hiyo Abdallah Mahmoud kuhakikisha anaendelea kusimamia kikamilifu kata, vijiji na Jimbo kuwa viti hivyo viendelee kuwa CCM na sio upinzani.
Ametoa maelekezo hayo mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa chama cha mapinduzi ngazi ya wilaya ambapo Mahmoud alichaguliwa kuwa mwenyekiti mpya kwa kupata kura 411 kati kura 447 huku 2 zikiharibika na akiwagaragaza wapinzani wake Omari Ally na Shafii Akida katika uchaguzi huo uliokuwa wa aina yake.
Rajab alisema kwamba wakati alipokabidhiwa nafasi ya uenyekiti alikumbana na changamoto kubwa ya baadhi ya kata na vijiji kuwa upinzani lakini baadaye alihakikisha vyama vya upinzani vinarudi CCM jambo ambalo walifanikiwa kwa asilimia kubwa kutokana na mshikamano na umoja uliokuwepo baina ya na wanachama.
"Nikupongeze ndugu yangu Mahamoud kwa kuchaguliwa leo kwa kishindo kuwa Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Pangani tambua kwamba katika majukumu yako unapaswa kuhakikisha kwamba chama cha mapinduzi CCM kinaendelea kushinda kwenye chaguzi zijazo ikiweno kura za Rais, Mbunge, Madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji, alisisitiza Mwenyekiti Mstaafu.
Alisema jambo hilo linaweza kufanikiwa iwapo wataendeleza umoja na mshikamano huku akiwataka viongozi wapya kuhakikisha wanaepukana na makundi ndani ambayo yanaweza kusababisha mpasuko miongoni mwao.
"Chama lengo lake ni kushika dola unapofika uchaguzi mkuu kwahiyo Mwenyekiti ulielewe una jukumu hilo mimi naondoka kwenye nafasi hii nakukabidhi vijiji vyote 33 viko chini ya chama cha mapinduzi na vitongoji vyote 96 viko chini ya chama cha mapinduzi naamini unapukuja uchaguzi wa mwaka 2024 wa vijiji na vitongoji kasi hii inaendelea kama ulivyoahidi,"alisema Rajab
Aidha alimkabidhi madiwani wa kata 14, Mbunge na Rais wote wanaotokana na chama cha mapinduzi na kumtaka ifikapo mwaka 2024/25 katika uchaguzi kasi hiyo iendelee na viongozi wote hao watokane na chama cha mapinduzi.
Amemsisitiza Mwenyekiti huyo mpya wa CCM kuhakikisha anakwenda kusimamia maendeleo ta wananchi wa Wilaya ya Pangani ili kuweza kuwainua kiuchumi wao na jamii zao na hivyo kuweza kujikwamua kimaisha.
Akitoa shukrani mara baada ya kuchaguliwa Mwenyekiti mpya alieyechaguliwa Rajab Mahmoud ameahidi kuanza kuzipatia ufumvuzi changamoto zinazowakabili makatibu wa matawi ikiwemo suala la usafiri ambapo ameahidi kuwapatia baiskeli makatibu wote 53 ili kuwarahisishia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Hatua hiyo inatokana na baadhi ya makatibu tawi kutembea umbali mrefu kuwafikia wananchi na hivyo wakati mwingine kushindwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi na tija kutokana na jiografia ya Pangani maeneo kuwa na umbali kutoka eneo moja kuja jingine.
"Mungu akinijaali kila mmoja nitampatia baiskeli moja moja kwakuwa kuna makatibu wa matawi wanatembea zaidi ya kilomita 9 kutimiza majukumu yao ya chama bila mshahara kwahiyo hili nimeliona na ndio jambo la kwanza ambalo nitaanza nalo huku mengine ya kukijenga chama chetu yakiendelea, "alisema Mahmoud
Mwenyekiti huyo alisema uchaguzi umekwisha hivyo kilichobaki ni kushirikiana na watu wote bega kwa bega ili kuhakikisha chama kinashika dola na kinashinda chaguzi zote bila kikwazo chochote.
Mbunge wa jimbo la Pangani ambaye pia ni Waziri wa maji Jumaa Aweso amewasihi viongozi waliochaguliwa katika nafasi zao kuhakikisha chama cha mapinduzi kinaendelea kushika dola na kuhakikisha mipango na malengo ya chama inafikiwa ikiwa ni kuisimamia serikali kuhakikisha inatimiza majukumu yake huku akiahidi kushirikiana na viongozi hao.
"Nimshukuru Rais Samia ambaye ni Mwenyekiti wetu wa chama cha mapinduzi Taifa kwani hakuna demokrasia yeyote ya kutafuta viongozi ndani ya chama zaidi ya uchaguzi hivyo kuanzia ngazi ya chini mpaka juu uchaguzi mbalimbali umefanyika, "alisema Mbunge Aweso.
Aliongeza kuwa ninaamini viongozi waliopatikana ni sahihi katika kuleta maendeleo ya wananchi na ndani ya chama hivyo niwasihi viongozi waliochaguliwa kuendeleza umoja na mshikamano ambavyo ndio silaha ya mafanikio, "alisisitiza Mbunge Aweso.
Akitangaza matokeo hayo Msimamizi wa uchaguzi huo mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Taifa Mohamed Ratco alisema katika uchaguzi huo nafasi ya Mwenyekiti kulikuwa na wagombea watatu ambao ni Omari Ally aliyepata kura 5, Shafii Akida kura 29 huku Abdalah Mahmod akiibuka mshindi kwa kupata kura 411 kati ya kura 447
Chama cha mapinduzi CCM Wilaya ya Pangani kimefanya uchaguzi wa viongozi mbalimbali wa nafasi ya uenyekiti, wajumbe mkutano mkuu wa Taifa na Mkoa.
MAHMOUD AIBUKA MSHINDI MWENYEKITI MPYA CCM WILAYA PANGANI
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 02, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 02, 2022
Rating:








Post a Comment