Mhe. Mchengerwa: chagueni viongozi watakaowaletea maendeleo wanarufiji
Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo na Mbunge wa Rufiji, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewaasa wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM Wilaya ya Rufiji kufanya maamuzi sahihi ya kuwachagua viongozi bora na waadilifu wataowaletea maendeleo ya kweli.
Mhe. Mchengerwa ambaye amekuwa mgeni rasmi kwenye mkutano uliofanyika leo Oktoba 3, 2022 Utete wilayani Rufiji amesema wanarufiji wana kiu ya maendeleo hivyo ni muhimu kufanya maamuzi sahihi.
"Rufiji tunayoikusudia ni Ile ya miaka ya 1960 ambayo Rufiji ilikuwa ikiheshimika kwa maendeleo katika nchi yetu" amefafanua Mhe. Mchengerwa
Amefafanua, kuwa katika miaka ya 1960, uchumi wa wananchi wa Rufiji ulikuwa juu huku wilaya hiyo ikiongoza katika kilimo cha pamba nchini na Afrika kwa ujumla huku shughuli za Uvuvi na Kilimo ziliweza kulisha Sehemu kubwa ya Tanzania.
Ameyataja maendeleo mengine katika kipindi hicho kuwa ni wilaya hiyo kuwa na viwanda mbalimbali, vyakula vya kutosha ambapo amefafanua kuwa nyakati hizo amekuwa akiziita " Nyakati za Kazi kazi".
Aidha, amesema katika kipindi hiki kifupi kumekuwa na maendeleo makubwa katika sekta za afya, elimu na miundombinu hali ambayo imesaidia kuboresha maisha ya wananchi.
"Ni vizuri tukakumbuka kabla ya uchaguzi hali ilikuwa ngumu, zaidi ya kata nane hakukuwa na shule, zahanati na hata umeme lakini leo ninavyosimama hapa kata takribani zote tumeshaleta huduma hizi muhimu na zilizobaki tutazimaliza katika kipindi kifupi kijacho kulingana na mikakati na mipango tuliyojiwekea" amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Ameongeza kuwa tayari zabuni kwa ajili ya kutengeneza barabara kwa kiwango cha lami kutoka Nyamwage hadi Utete imetangazwa na utekelezaji wake unatarajiwa kufanyika katika kipindi kifupi inavyowezekana.
Pia katika mkutano huo, Mhe. Mchengerwa ameridhia kukarabati ukumbi wa mikutano wa wilaya na ofisi zote za chama katika kiwango cha kisasa huku akitoa usafiri wa pikipiki kwenye kata zote, Jumuiya zote na baiskeli 4 kwenye kila tawi ili kusaidia utekelezaji wa kazi za chama.
Katika hatua nyingine Mhe. Mchengerwa amewataka wajumbe wa mkutano huo kutanguliza upendo na mshikamano baina yao ili kujiletea maendeleo.
Mhe. Mchengerwa: chagueni viongozi watakaowaletea maendeleo wanarufiji
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 02, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 02, 2022
Rating:




Post a Comment