Header AD

header ads

BANDARI TANGA YAANDAA MIKAKATI YA KIMASOKO KUVUTIA WATEJA.


Na Hadija Bagasha Tanga, 

Mamlaka ya bandari Tanzania TPA Mkoa Tanga imeandaa mikakati mikubwa ya kimasoko itakayotekelezwa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa gati mbili za kisasa na maboresho ya kina cha bahari. 

Mikakati hiyo inayoandaliwa ni pamoja na kupunguza gharama kwa muda maalumu (Low Cost) ili kuwavutia wateja pamoja na kufanya mazungumzo na kuwashawishi wamiliki wa meli kuanza kuleta meli kubwa bandari ya Tanga badala ya kutumia bandari jirani. 


Hayo yamebainishwa na Meneja wa Bandari ya Tanga Masoud Mrisha wakati waandishi wa habari za kiuchumi, biashara na uwekezaji walipotembelea bandari hiyo na kujionea maboresho yanayoendelea katika bandari hiyo wakiongozwa na Bertha Mwambela wa TBC pamoja na Mussa Juma wa kampuni ya Mwananchi Communication. 

Meneja Mrisha amesema kuwa serikali kupitia mamlaka ya bandari Tanzania (TPA) inatekeleza mradi huo mkubwa wa kimakakati wa maboresho makubwa katika bandari ya Tanga ili iweze kuchangia kikamilifu katika kukuza pato la Taifa kwa kuhudumia wateja wa ndani na nchi jirani ambazo zinategemea bandari za Tanzania kusafirisha bidhaa kutoka na kwenda nje ya nchi. 


"Mikakati yetu ya kimasoko baada ya kukamilika kwa ujenzi huu ni pamoja na kuitangaza bandari ya Tanga kwa kutumia vyombo vya ndani kama Radio na luninga na kuonyesha makala maalumu (Documentaries), nje ya nchi kwa kutumia watumishi wa bandari waliopo nchi tunazohudumia (Liaison Officer) pamoja na balozi zetu nchi mbalimbali kuitangaza bandari ya Tanga na ndio wakati maalumu wa kurugenzi ya masoko kufanya mazungumzo na kuwashawishi wamiliki wa meli kuanza kuleta meli kubwa katika bandari yetu ya Tanga, alisisitiza Mrisha. 


Aidha Meneja Mrisha amesema matarajio yao baada ya mradi wa naboresho ya bandari ya Tanga kukamilika kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali katika mradi wa maboresho ya bandari hiyo mradi huo utakapokamilika utakuwa na faida mbalimbali ikiwemo uwezo wa bandari ya Tanga wa kuhudumia shehena utaongezeka kutoka tani 750,000 mpaka tani 3,000,000.


Pia alisema kuwa pamoja na kuongezeka kwa shehena kutakuwa na kuongezeka kiwango cha kodi inayokusanywa kutokana na shehena itakayosafirishwa kupitia bandari ya Tanga, kuongezeka kwa pato la Taifa, kufunguka kwa fursa nyingi za kiuchumi kwa mikoa ya Kaskazini mwa Tanzania pamoja na nchi jirani, kupungua kwa ghatama za uendeshaji wa bandari kutokana na kuondokana na gharama za double handling lakini pia kuongezeka kwa ufanisi na tija katika utendaji wa bandari. 

Meneja Mrisha amebainisha baadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo katika bandari hiyo ikiwemo uhaba wa eneo la kufanyia kazi ndani ya bandari ya Tanga, kutokuwa na Oil terminal na Tank farm bandari ya Tanga inayopelekea upotevu mapato kutokana na kampuni ya GBP kuimikili miundombinu hiyo hivyo tayari mamlaka ya bandari imeanza upembuzi yakinifu kwa mwaka fedha 2023/24 mradi huo utapewa kipaumbele kutekelezwa. 



"Changamoto nyingine ni treni kutoingia ndani ya bandari ya Tanga hivyo juhudi za serikali zinazoendelea za kufufua miundombinu ya reli ya TRC ndani ya bandari ya Tanga, "alisisitiza Meneja Mrisha. 

Kwa upande wake Mstahiki Meya wa jiji la Tanga Abdulrahman Shiloo amesema kuwa serikali kupitia TPA imelenga kuiboresha bandari ya Tanga ili kuwarahisishia wateja waliokuwa wanalalamikia changamoto ya kina kifupi na kutokuwepo kwa meli za moja kwa moja katika bandari hiyo. 

"TPA imelenga kuifanya bandari ya Tanga kuhidumia soko la Mikoa ya Kaskazini ikiwemo Mkoa wa Kilimanjaro, Arusha, Manyara, pamoja na nchi jirani za Rwanda, Burundi, DR Congo, Uganda na kenya.  

"Ndugu zangu waandishi wa habari naomba niwaambieni kwamba upanuzi wa bandari ya Tanga ni mpango mkakati wa serikali ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania ya awamu ya 6 chini ya mheshimiwa Samia Suluhi Hasan kuhakikisha kwamba anatengeneza, ajira kwa vijana animarisha uchumi na kuuborwsha uchumi wa nchi lakini pia kuongeza pato la Taifa na bandari hii ni miongoni mwa bandari kongwe kati ya bandari za Afrika mashariki, "alisema Meya Shiloo. 

Baada ya kukamilisha maboresho yanayoendelea, matarajio ya bandari ya Tanga ni kuhudumia tani za mapato zipatazo milioni 3.

Lengo la mradi huo ni kuboresha magati mawili yenye urefu wa mita 450, kuongeza mita 50 upande wa mashariki na mita 92 upande wa magharibi kuelekea baharini ikiwa ni pamoja na kuongeza kina cha maji kutoka mita 3 hadi 13.

Mpaka sasa mradi huo umefikia asilimia 82 na tayari wamekabidhiwa kipande chenye urefu wa mita 300 na hivyo kubakiwa na mita 150 ili mradi wote ukamilike.



BANDARI TANGA YAANDAA MIKAKATI YA KIMASOKO KUVUTIA WATEJA. BANDARI TANGA YAANDAA MIKAKATI YA KIMASOKO KUVUTIA WATEJA. Reviewed by Fahadi Msuya on December 30, 2022 Rating: 5