Header AD

header ads

Sintofahamu yaibuka Morogoro wananchi wakimbia makazi yao

 


Na Mwandishi wetu 

WANANCHI wa kijiji cha Merela kata ya chita halmashauri ya Mlimba wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro wameiomba Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuingilia kati mgogoro wa ardhi unaopelekea jamii kukimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wao.

Mgogoro huo ambao unadaiwa kumuhusisha mwekezaji mtanzania na wananchi kwa madai ya kuwa moja ya eneo katika kijiji hicho lenye ukubwa zaidi ya Hekari 2000 ni sehemu yake jambo ambalo wananchi wamelipinga kwa madai wameishi hapo zaidi ya miaka 20 wakiwa wanaendelea na shughuli zao za kilimo na ufugaji bila changamoto yoyote ile.


Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Merela halmashauri ya Mlimba akijulikana kwa jina la Kiliani Nyahororo alisema wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya kikatili ikiwemo baadhi ya wanawake kuingiliwa kimwili bila ridhaa yao na wanaodaiwa ni maofisa wa polisi ili kuondoka eneo hilo, jambo ambalo limezua taharuki kubwa kwa jamii kukimbia makazi kwa kuhofia usalama wao

"kuna familia ya wakazi zaidi ya 1000, mpaka sasa hivi tunaomba serikali itusaidie kwa hili, hatulali ndani, wake zetu wanalala nyumbani mara nyingine wanabakwa, hatuna msaada kwenye ofisi ya kijiji, wilayani mpaka mkoani" alisema Nyahororo


Aidha, baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walifungua kesi ya kupinga mwekezaji huyo kuendelea kutumia eneo hilo, sintofahamu iliibuka baada ya miezi kadhaa mwekezaji huyo kurudi kijijini hapo nakudai kuwa mahakama imeshatoa hukumu kuwa yeye yupo kisheria kumiliki eneo hilo, jambo ambalo wananchi hao wadai kuwa kesi bado inaendelea na hukumu haijatolewa.

Kwa upande wake kaimu Mwenyekiti wa kijiji cha Merela Hashimu Ngwembe alisema Serikali ya kijiji hicho haitambui mgogoro huo, kwa sababu mahakama ilishatoa hukumu kwa kumuagiza mwekezaji aendelee na shughuli zake katika eneo lenye Hekari 2000 kwenye kitongoji cha Msondo.


"serikali ya kijiji hatuna mgogoro na mwekezaji tunaamini mwekezaji yupo kisheria, ndio maana hata kwenye mahakama zilizozungumzwa hizi kesi hukumu zake zilitoka kuwa mwekezaji aendelee na shughuli zake, pia wananchi, mwekezaji na serikali ya kijiji tulishakubalina ila kuna baadhi ya watu wachache ambao wao wanaona bado wanahaki ya kuendelea kuwa sehemu hiyo ya mwekezaji" alisema kaimu mwenyekiti Ngwembe

Hivyo, naye kamanda wa polisi mkoa wa Morogoro Fortunatus Muslimu alisema jeshi la polisi linafanya doria za kawaida kutafuta wahalifu na sio kuondoa wananchi kwenye maeneo hayo.
Sintofahamu yaibuka Morogoro wananchi wakimbia makazi yao Sintofahamu yaibuka Morogoro wananchi wakimbia makazi yao Reviewed by Fahadi Msuya on December 13, 2022 Rating: 5