Header AD

header ads

TET YAANZA UFUATILIAJI MPANGO WA UTAYARI WA KUMUANDAA MTOTO KUANZA SHULE PWANI



Taasisi  ya Elimu Tanzania (TET) kupitia  Programu ya Shule Bora, leo tarehe 19/12/2022 imeanza kufanya ufuatiliaji katika  vituo mbalimbali vya Mpango wa Utayari wa kumuandaa Mtoto kuanza Shule  katika  Mkoa wa Pwani.

Vituo hivyo vya utayari vilianza mwezi Oktoba mwanzoni mwaka huu ambapo watoto watahudhuria kwa wiki kumi na mbili hadi mwishoni mwa mwezi huu kabla ya kuanza darasa la kwanza  mwaka 2023.

Akizungumza katika Wilaya ya Bagamoyo kwenye  vituo vya Utayari  vya Kudibahi na Mikoroshini, Mkurugenzi wa Mafunzo ya Mitaala, Dkt. Fika Mwakabungu amesema kuwa ameridhishwa na namna vituo hivyo vinavyoendesha madarasa hayo ya utayari na kuwa watoto walioweza kuhudhuria wamejifunza na kuwa tayari kuanza darasa la kwanza.


“Kwa kweli kazi kubwa imefanyika kwani watoto wanaonekana kabisa kuelewa kile walichofundishwa na hii imewajengea kujiamini na kuonesha sasa wako tayari kuanza masomo yao ya msingi na kuwa kama watoto wengine walioweza kupitia madarasa ya awali” amesema Dkt. Mwakabungu.

Dkt.Mwakabungu amewapongeza  Walimu Wasaidizi wa Jamii wote waliokubali jukumu la kuwaandaa watoto hao katika  vituo vyote vya mkoa wa Pwani pamoja na wazazi wote walioweza kuruhusu watoto wao kuandaliwa katika vituo hivyo na amesema kuwa anaamini mwakani watoto wengi wataweza kuletwa katika vituo mbalimbali vya utayari.

Kwa upande wake mwakilishi wa  walimu wa vituo hivyo  Bi.Neema Taigo amesema kuwa wanafunzi wameonesha uelewa mkubwa katika  madarasa hayo  na kuwa katika mwaka ujao watoto wengi wataweza kujitokeza kwa wingi.

Naye mwakilishi wa wazazi Bwana. Richard Kwiyela  ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuhakikisha Elimu inapatikana kuanzia ngazi ya chini na kwamba, wakazi katika eneo lao watashirikiana na serikali katika kuhakikisha wanajenga shule  kuanzia elimu ya Awali hadi Msingi ili kuhakikisha watoto wote wanapata elimu kama wengine.



Mbali na Wilaya ya Bagamoyo, leo pia katika wilaya ya Kibaha DC na Rufiji vituo vya utayari vya Ruvu Dosa, Mnazi,  Nyabhanje na Ngomboroni viliweza kutembelewa na  kuonekana maendeleo yake na utekelezaji ulivyofanyika wa Mpango wa  Utayari.

Mpango huo wa vituo  vya Utayari unataekelezwa na Ofisi ya Rais -TAMISEMI kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania(TET) chini ya mradi wa Shule Bora .
TET YAANZA UFUATILIAJI MPANGO WA UTAYARI WA KUMUANDAA MTOTO KUANZA SHULE PWANI TET YAANZA UFUATILIAJI MPANGO WA UTAYARI WA KUMUANDAA MTOTO KUANZA SHULE PWANI Reviewed by Fahadi Msuya on December 19, 2022 Rating: 5