Header AD

header ads

UWT YAPONGEZA UAMUZI WA RAIS DKT. SAMIA KUONDOA ZUIO LA MIKUTANO YA HADHARA



Na Hadija Bagasha Tanga, 

Mwenyekiti wa umoja wa wanawake Tanzania (UWT) Mary Chatanda amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kufanya maamuzi ya kuondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa hatua iliyokwenda kutoa majawabu ya vikwazo vya demokrasia Nchini. 

Kufuatia uamuzi huo Chatanda amewataka viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa kuanzia ngazi za chini kufanya mikitano ya hadhara  kwa kufanya siasa za kistaarabu,  kujenga hoja zenye ushawishi katika uendeshaji wa nchi na si kutumia majukwaa hayo kufanya siasa za matusi na kashfa. 


Chatanda ametoa pongezi hizo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Tanga ikiwa ni siku moja tu mara baada ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutoa tamko la kuondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama siasa tamko linalotajwa kuwa limeleta faraja kwa vyama vya siasa Nchini. 

"Sisi UWT tumekoshwa sana na hatua ya kihistoria ya kuondoa zuio la mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa,  kukwamua mchakato wa kupata katiba mpya,  kufanya marekebisho ya sheria mbalimbali ili kupanua wigo wa demokrasia hapa nchini maamuzi haya ya Dkt Samia Suluhu Hassan yameleta faraja hususani kwa vyama mbalimbali vya siasa hapa nchini, "alisema Chatanda. 


Aidha Dkt Samia ameendelea kuonyesha kwa vitendo kauli zake hivyo wanaungana na wito wa Rais kwa wanasiasa kutumia ruksa ya mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa kufanya siasa za kistaarabu za kupevuka na zenye kujenga nchi na zisizokuwa na matusi na kashfa. 

"Dkt Samia ni kiongozi msikivu,  mkweli na mpenda haki na ndio maana maamuzi matatu yaliyochukuliwa na Rais Samia jana kwa vyama vya siasa ni mwelekeo mpya wa nchi yetu katika kukuza demokrasia yetu UWT tunasema hakika mama Samia ni neema kutoka kwa Mungu, "alisisitiza Chatanda. 


Sambamba na hayo Mwenyekiti Chatanda amesema kilio chao UWT siku zote ni kuona nchi ikiwa na utulivu,  amani na yenye haki baina ya wananchi wake na serikali yao kwani Rais Samia ameonyesha njia hivyo ni wajibu wao wote wanasiasa, wananchi na viongozi wengine kufuata kwa unyenyekevu maamuzi  yake na si kumkatisha tamaa. 

Alisema UWT inawasihi viongozi wote wanawake  ndani ya vyama siasa kuonyesha mfano katika hilo kwa kutanguliza ustaarabu kuheshimiana,  utu wakati wote wa mikutano ya hadhara na kamwe pasitokee viongozi wa vyama vya siasa kubeza na kutweza utu wa mwanamke na mtu mwingine katika mikutano hiyo ya vyama vya siasa. 


Kwa upande wake mjumbe wa Halmashauri kuu ya ccm Taifa (MNEC)  Mohamed Salim Ratco amempongeza Rais Dkt Samia kwani tokea aingie madarakani kwa muda mfupi ameweza kufanya mambo makubwa hususani katika masuala ya kidemokrasia nchini. 


Ratco alisema matarajio yao kama vyama vya siasa ni kuona panafanyika siasa za kistaarabu kuanzia ngazi za tawi,  kata, wilaya na Taifa ikiwa ni pamoja na kuyasema mazuri yote yaliyotekelezwa katika ilani ya chama cha mapinduzi ccm. 

"Nidhamu ichukue mkondo wake na siasa zina mipaka tumewahi kushuhudia kiongozi mmoja wa vyama vya upinzani akizungumza mambo ambayo si mazuri akafunguliwa kesi akashindwa baadae akaomba radhi kwahiyo hatutarajii hayo yatokee lengo letu kukosoana pale ambapo tumefanya makosa tuwekane sawa na sio kutumia lugha za kashfa matusi na kukebehi, "Alisema Ratco. 

Kituo hiki kilifika ofisi za chama cha wananchi CUF ili kujionea namna walivyolipokea agizo hilo ambalo linakwenda kuonyesha mwanga kwa vyama vya upinzani na kukutana na Mwenyekiti wa chama hicho Khamisi Mnyeto ambaye amesema chama hicho kimefurahishwa na maamuzi ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwani sasa demokrasia ya kweli nchini inakwenda kufanyika. 

Hata hivyo aliyekuwa Mbunge wa jimbo la Tanga kupitia chama cha wananchi CUF Mussa Mbarouk amesema kuwa uliokuwa ukifanyika ni ukandamizaji wa demokrasia Nchini licha ya kwamba  jambo hilo lilikuwa la kikatiba na kisheria. 


"Hili ni jambo jema sana na la kufurahia sana wanasiasa tulijiona kama tumefungiwa kwenye chumba hii fursa tuitumie vizuri kwa kunadi sera zetu ili tuweze kuongeza wanachama na wananchi tuwaeleze nchi yetu inatoka wapi na inakwenda wapi, "alibainisha Mbarouk. 


UWT YAPONGEZA UAMUZI WA RAIS DKT. SAMIA KUONDOA ZUIO LA MIKUTANO YA HADHARA UWT YAPONGEZA UAMUZI WA RAIS DKT. SAMIA KUONDOA ZUIO LA MIKUTANO YA HADHARA Reviewed by Fahadi Msuya on January 04, 2023 Rating: 5