Header AD

header ads

CHONGOLO KUHUTUBIA MAELFU YA WANANCHI WA TANGA



Na Hadija Bagasha Tanga, 

Katibu Mkuu wa chama cha mapinduzi ccm Daniel Chongolo anatarajiwa kuhutubia maelfu ya wakazi wa Mkoa wa Tanga katika mkutano utakaofanyika kwenye viwanja vya shule ya msingi mazoezi akiongozana na wataalamu wabobezi wa masuala ya uwekezaji mahali ambapo jamii itaelimishwa ipasavyo juu ya sakata la uwekezaji kwenye bandari ya Daresalaam na serikali ya falme ya Dubai. 


Katika mkutano wa waandishi wa habari uliohudhuriwa na wabunge,  wakuu wa wilaya, viongozi wa chama, na dini,  Mkuu wa wilaya hiyo Jokate Mwegelo amesema mkutano huo unakwenda kuondoa sintofahamu iliyosababishwa na, baadhi ya watu wasioitakia mema Tanzania. 


"Tumuunge mkono mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan sisi tumepokea ugeni wa ujio wa katibu Mkuu wa chama cha mapinduzi Comred Daniel Chongolo anakuja yeye lakini anakuja na wataalamu wabobezi wa sheria waliolitengeneza hili jambo waliosomeshwa na jamuhuri ya Muungano wa Tanzania watakuja kutuelezea kinagaubaga ukweli wa hili jambo na jinsi ambavyo linakwenda kutekelezwa, "alisema DC Jokate

Aidha Jokate amesema kuwa wananchi wanapaswa kujitokeza kwa wingi huku wakiwa na utayari wa kupokea ukweli ambao utawasilishwa na wataalamu wabobezi na wenye uzoefu hususani katika masuala ya kiuchumi,  uwekezaji na masuala ya kinchi. 

"Tunataka kila mwananchi sasa apate nukta yake sio nukta ya kujazwa na propaganda ya kujazwa hofu ya kujazwa maneno njoeni kesho viwanja vya mazoezi ili iwe ni ishara ya kumuonyesha mheshimiwa Rais kwamba tuko naye bega kwa bega lakini pili iwe ni ishara ya kwamba tuko tayari kuelimishwa juu ya suala hili ili tuondokane na upotoshwaji na tuondokane na kauli za mtaani na pia tuondokane na sintofahamu, "alisisitiza DC Jokate. 

Mkuu  wa wilaya ya Tanga James Kaji na Mkuu wa wilaya ya Handeni Wakili Albert Msando  wakiwa kwenye mkutano huo wamesema uwekezaji  umetokana na makusanyo ya bandari ya Daresalaam na kufanya viongozi wakuu wa nchi kuona umuhimu wa kutafuta mwekezaji. 



"Bandari kwetu imekuwa ndio langu kuu la kiuchumi hasa bandari ya Daresalaam,  Tanga na nyinginezo tukiangalia historia kidogo bandari zetu hazifanyi kazi vizuri na hazina mafanikio sana ni kwanini hali hii ndio imepelekea mheshimiwa Rais pamoja na watawala wake na baraza la mawaziri kuamua kutafuta mwekezaji, "alisema Kaji. 

"Wale ambao wanajaribu kupotosha au kusema tofauti kwanza watambue hii sio ligi ya kushindana nani anajua kusema sana na nani hajui tunachokifanya sisi ni kuzungumzia au kusema mustakabali wa nchi yetu maslahi ya nchi yetu na nini watanzania wanakitaka kutoka kwetu sisi ambao tumepewa dhamana ya uongozi, "alisema Wakili Msando. 

Mbunge wa Korogwe mji Dk Alfred Kimea na Mbunge wa Korogwe vijijini Timotheo Mzava wamesema bunge lilikubali  uwekezaji huo baada ya kuona una manufaa nakubwa kwa Taifa. 



"Kimsingi nimejiridhisha kabisa pasipo na, mashaka kwamba makubaliano yale kati ya serikali yetu na serikali ya Dubai yanakwenda kuwa na manufaa makubwa kwa nchi yetu ya Tanzania, "alisema Kimea

"Limekuka jambo la bandari wenzetu wamepata agenda wanapita kila mahali wanaita vyombo vya habari kila siku wanazungumzia jambo hilo na ili iwe agenda kwao ni lazima waiseme kwa namna ambayo inaweza ikawafurahisha wao lakini inatoa ukweli na uhalisia wa jambo husika sisi kama Wabunge tulipitisha azimio hilo tukiwa na akili timamu tukiwa tumelifanyia kazi ya kutosha tukiwa tumejiridhisha kwamba ni azimio ambalo tukilipitisha makubaliano yale yanakwenda kusaidia mustakabali mzuri wa Taifa letu, "alisema Mzava. 

Hatua ya Mkutano huo imekuja mara baada ya kuwepo kwa taarifa tofauti  dhidi ya uwekezaji huo huku serikali ikisema hatua hiyo itasaidia kuongeza ufanisi kwenye bandari ya Daresalaam na kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa. 


CHONGOLO KUHUTUBIA MAELFU YA WANANCHI WA TANGA CHONGOLO KUHUTUBIA MAELFU YA WANANCHI WA TANGA Reviewed by Fahadi Msuya on July 18, 2023 Rating: 5