MAJALIWA AZINDUA MUONGOZO WA FURSA ZA UWEKEZAJI MKOA WA TANGA
Tanga
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amezindua kitabu cha muongozo wa fursa za uwekezaji katika mkoa wa Tanga na kutoa maagizo manane ikiwemo kuondoa urasimu usiokuwa wa lazima unaokatisha tamaa wawekezaji.
Pia amesema mtumishi yeyote anayekwaza sekta binafsi wanaowekeza hapa nchini ni adui mkuba wa uchumi wa nchi kwavile duniani kote hakuna nchi ambayo imepiga hatua kiuchumi bila kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Waziri wa Nchi katika ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo, alisema Mkuu wa mkoa ashirikiane na kituo cha uwekezaji (TIC) kuhakikisha wawekezaji wote wanatumia muda mfupi kadiri iwezekanavyo kukamilisha mchakato wa uwekezaji.
Alisema falsafa inayomuongoza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuleta fursa za uwekezaji, maono yake ni kufungua nchi kiuchumi.
Alisema serikali haitengenezi fedha bali inajenga mazingira na kutoa fursa kwa wawekezaji ambao wanatengeneza ajira zinazotoa wigo kwa Watanzania kufanya kazi na kujenga uchumi wa nchi.
"Rais anaposema anafungua nchi maana yake ni kuweka mazingira bora ya uwekezaji watu wapate ajira kwasababu serikali haitengenezi fedha, fedha zinatengenezwa na wawekezaji, hivyo tuna wajibu mkubwa wa kusimamia na kuweka mazingira yatakayowasaidia katika shughuli zao siyo kuwakwaza," alisema.
"Nchi zote zilizoendelea na kupiga hatua na kufika katika uchumi wa kati kama nchi za Mauritius, Botswana na Afrika Kusini, ziliweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara na wawekezaji.
Alisema kuna mambo matatu ambayo yamekuwa yakiwakwanza wawekezaji ambayo ni mlundikano wa sheria (Over Regulations), urasimu wa watendaji na suala la miundombinu.
"Watumishi wa umma lazima wabadilike wawe marafiki wa wafanyabiashara, wanapokwama wawaelekeze bila kuwakwaza, suti hizi tunazovaa zinatokana na kodi wanazolipa," alisema.
Maagizo mengine ya Waziri Mkuu ni pamoja na kuwaagiza mamlaka za serikali za mitaa kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji na kuyawekea miundombinu yote, mkoa uwaandae mawasiliano ili kuongeza fursa za uwekezaji.
Lakini pia Waziri Mkuu, alisema mipango yote ya uwekezaji izingatie dhamira ya Serikali ya uhifadhu na utunzaji wa mazingira na mkoa usimamie suala la uvunaji endelevu wa mazao ya bahari.
Pia aliagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini, wekeni mikakati ya utekelezaji wa fursa zilizopo katika maeneo yenu wakitumia miongozo ya mikoa sambamba na kubainisha fursa mpya za uwekezaji.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Tanga Waziri Kindamba amesema kongamano hilo kubwa la uwekezaji kunatokana na maboresho makubwa ya Bandari ya Tanga, kutambua fursa zilizopo mkoani hapa.
Alisema lengo la Kongamano hilo ni kutambua fursa za kiuwekezaji za zao la biashara la Mkonge sanjari na kutambua mradi mkubwa wa Bomba la mafuta ghafi kutoka Hoima nchini Uganda linalojengwa Chongoleani,ikiwemo fursa nyingine za kiuchumi zilizpo mkoani humo.
Katika Kongamano hilo benki ya NMB imeshirikiki Kongamano la Uwekezaji wa Biashara huku wakibainisha kwamba kwa hivi sasa mwekezaji mkubwa anaweza kuchukua mkopo mpaka bilioni 340 kwa mkopaji mmoja.
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kaskazini Baraka Ladislaus amesema kwamba kupitia kongamano hilo wawekezaji wanaweza kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo ili kuweza kujikwamua kiuchumi ambao utakuwa chachu ya kukuza pia mitaji yao na hatimaye kuweza kuchochea ukuaji wa biashara zao.
“Wenzetu wa Simba kama mtaji ni changamoto karibuni sana lakini uwekezaji huo wa Tanga hauwezi kuwezekana bila kuwa na upatikanaji wa huduma za kifedha na wana matawi ya benki zaidi ya 12 kwa wilaya zote nane na wilaya nyengine wana matawi mawili na hivyo hii ni kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha tunazoziongelea”Alisema
Hata hivyo alisema kwamba benki hiyo wamejipanga vizuri na itaendelea kushirikiana na Serikali ili kuchangiza maendeleo muhimu kwa watanzania .
Meneja huyo wa Kanda aliwaeleza wawekezaji watanzania waliopo mkoani Tanga kwamba benki hiyo inajivunia kushiriki kwenye kongamano na wanataka kuwaambia wawekezaji wa Tanga kwamba inajivunia uwezo wake mkubwa kuwahudumia sekta mbalimbali za uwekezaji na wameanza kuhudumia sekta ya biashara za kati na wadogo kwa kuwa na muda mrefu wa kuwahudumia.
Hata hivyo alisema kwamba pia benki hiyo imeendelea kukuza mtaji wake na niwaambie wawekezaji kwamba benki ina uwezo mkubwa wa kutoa mitaji ambayo itachagiza uwekezaji ambao unaozungumziwa leo ambao umekuwa mkombozi kwao.
MAJALIWA AZINDUA MUONGOZO WA FURSA ZA UWEKEZAJI MKOA WA TANGA
Reviewed by Fahadi Msuya
on
November 16, 2023
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
November 16, 2023
Rating:






Post a Comment