BoT Yatangaza Zoezi la Kubadilisha Noti za Zamani, Kuanza Januari 6, 2025
![]() |
| Kaimu Mkurugenzi Usimamizi wa Sarafu BoT, Ilulu Ilulu akionesha fedha ambazo zinatumika kwasasa pamoja na fedha za zamani ambazo zinahitajika kuondolewa kwenye mzunguko, alipokutana na waandishi wa habari leo Oktoba 31, 2024 kutoa taarifa ya mpango wa kuondoa noti za zamani katika mzunguko wa sarafu. |
Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza rasmi kuanza kwa zoezi la kubadilisha noti za zamani kuanzia Januari 6, 2025. Zoezi hili litadumu kwa miezi mitatu, hadi Aprili 5, na wananchi wametakiwa kuziwasilisha noti hizo benki ili kuzipata thamani yao halisi kabla ya mwisho wa kipindi hicho.
Kaimu Mkurugenzi wa Usimamizi wa Sarafu BoT, Ilulu Ilulu, alieleza mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mnamo Oktoba 31, 2024, kwamba mchakato huu utafanyika katika ofisi zote za Benki Kuu pamoja na benki za biashara kote nchini. Wananchi wataweza kupatiwa malipo kulingana na thamani halisi ya noti walizowasilisha.
Ilulu alisisitiza umuhimu wa kuhakikisha kwamba wananchi wanawasilisha noti zilizo halali, ambazo zina alama za usalama zinazotambulika. Alieleza kuwa kufanikisha zoezi hili ni njia ya kuhakikisha Watanzania wanapata thamani kamili ya fedha zao, badala ya kuzikosa kutokana na noti hizo kuondolewa kwenye mzunguko rasmi.
"Inapotokea kusitisha uhalali wa noti fulani, wananchi hupewa muda maalumu wa kuzibadilisha kabla ya uhalali huo kuondolewa kabisa. Hii ni fursa kwao kupata kiwango kilekile cha thamani walichonacho," alisema Ilulu.
Aidha, Ilulu aliwataka wananchi kuepuka kuuza au kununua noti chakavu mitaani, akibainisha kuwa kitendo hicho ni kosa kisheria na mara nyingi hufanywa na matapeli. Alieleza kwamba BoT imefungua madirisha maalumu kwenye benki zote za biashara nchini ili kuwezesha zoezi hili.
“Suala la kununua na kuuza sarafu halipo kisheria, kwani kinachofanyika hapo ni utapeli kwa kutokujua taarifa. BoT imetoa fursa kwa benki zote za biashara nchini kuwa na dirisha la kubadilisha noti chakavu,” aliongeza.
Kwa mujibu wa BoT, noti zinazohitajika kuondolewa kwenye mzunguko ni shilingi ishirini (20), mia mbili (200), mia tano (500), elfu moja (1,000), elfu mbili (2,000), elfu tano (5,000), na elfu kumi (10,000) zilizotolewa kati ya mwaka 1985 na 2003, pamoja na noti ya mia tano (500) ya mwaka 2010. Sifa za noti zinazostahili kubadilishwa zimeainishwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 858 la Oktoba 11, 2024.
Wananchi wametakiwa kufika benki na kutumia dirisha lililofunguliwa kwa ajili ya huduma hii ili kunufaika na zoezi hili muhimu.


(PICHA ZOTE NA EMMANUEL MBATILO)
Reviewed by Fahadi Msuya
on
November 03, 2024
Rating:

Post a Comment