Misaada kwa Wahanga wa Kariakoo Kupitia Akaunti Rasmi
Dar es Salaam, Novemba 18, 2024 – Serikali imeelekeza kuwa misaada yote ya kifedha kwa ajili ya kusaidia waathirika wa kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo itapokelewa kupitia Akaunti Maalumu ya Maafa 9921159801, iliyopo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) chini ya usimamizi wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonazi, amesema akaunti hiyo imethibitishwa rasmi na serikali kuwa njia pekee ya kupokea michango ya kifedha kwa ajili ya maafa.
“Kuna watu wana nia njema kabisa ya kusaidia waathirika wa tukio hili, lakini tunawaomba wote wajiepushe na kukusanya michango kutoka kwa watu binafsi au vikundi bila kupitia akaunti hii maalumu,” alisema Dkt. Yonazi.
Akaunti hiyo, kwa mujibu wa serikali, imelenga kuhakikisha misaada inawafikia walengwa kikamilifu na kwa uwazi, huku ikihakikisha malengo ya msaada huo yanatimizwa bila changamoto za kiutendaji au kiufisadi.
Dkt. Yonazi pia alibainisha kuwa zoezi la uokoaji bado linaendelea katika eneo la tukio, huku juhudi zikiwa zimeelekezwa katika kuokoa watu ambao bado hawajapatikana.
Tukio la kuporomoka kwa ghorofa Kariakoo limeibua mshikamano mkubwa kutoka kwa Watanzania na jamii ya kimataifa, huku misaada ya kifedha na vifaa ikitarajiwa kusaidia waathirika na kurudisha hali ya kawaida kwa walioathirika na tukio hilo.
Serikali inawataka wananchi na taasisi zote zinazotaka kusaidia kuhakikisha michango yao inafikishwa kupitia akaunti rasmi ili kuwezesha uratibu wa misaada kufanyika kwa ufanisi.
Misaada kwa Wahanga wa Kariakoo Kupitia Akaunti Rasmi
Reviewed by Fahadi Msuya
on
November 18, 2024
Rating:


Post a Comment