Header AD

header ads

CRDB NA FAO WAUNGANA KUBORESHA KILIMO ENDELEVU NCHINI





Katika kuendelea kusherehekea miaka 30 ya uongozi katika sekta ya fedha nchini, Benki ya CRDB imeingia makubaliano ya ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO). Ushirikiano huu unalenga kusaidia wakulima wadogo kufanya kilimo stahimilivu kwa mabadiliko ya tabianchi, kupunguza vihatarishi, na kukuza ufadhili wa kilimo endelevu nchini kupitia teknolojia za kisasa.


Akizungumza katika hafla ya utiaji saini iliyofanyika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisisitiza utayari wa benki hiyo kuwawezesha wakulima kufanya kilimo cha kisasa. “Sisi kama Benki ya CRDB tunajivunia kuwa benki pekee nchini yenye usaili wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (UN GCF), jambo linalotuwezesha kuwekeza zaidi katika miradi ya kilimo endelevu na kusaidia wakulima kukabiliana na changamoto za tabianchi,” alisema Nsekela.


Kupitia ushirikiano huu, Benki ya CRDB na FAO zitatengeneza suluhisho za kifedha zinazolenga kuboresha maisha ya wakulima wadogo na kuimarisha uzalishaji wa chakula nchini. Mpango huu pia unachangia ajenda ya Serikali ya 10/30, inayolenga kukuza sekta ya kilimo na kuhakikisha inachangia asilimia 10 ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania ifikapo mwaka 2030.


Hii ni mara ya kwanza kwa FAO kuingia makubaliano ya aina hii na taasisi za fedha barani Afrika, hatua inayoonesha dhamira ya CRDB katika kusaidia sekta ya kilimo. Kwa sasa, Benki ya CRDB inaongoza nchini kwa uwezeshaji wa sekta ya kilimo, ikitoa asilimia 60 ya mikopo yote ya kilimo nchini.


Kwa ushirikiano huu wa kimkakati, wakulima wadogo wanatarajiwa kupata fursa bora za kifedha, zana za kisasa za kilimo, na elimu kuhusu mbinu bora za kilimo endelevu, hatua itakayosaidia kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula nchini.

CRDB NA FAO WAUNGANA KUBORESHA KILIMO ENDELEVU NCHINI CRDB NA FAO WAUNGANA KUBORESHA KILIMO ENDELEVU NCHINI Reviewed by Fahadi Msuya on February 20, 2025 Rating: 5