NMB yakabidhi Gawio la Bil. 68.1/- kwa Serikali, Msajili Hazina aipongeza
Pongezi hizo zimetolewa na Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, wakati wa hafla ya Gawio Day, ambako Rais Dk. Samia Suluhu Hassan alikuwa akipokea gawio na michango ya jumla la Sh. Trilioni 1.28 kutoka kwa Mashirika, Taasisi za Umma, na Kampuni ambazo Serikali ina Hisa chache.
Akizungumza kabla ya kukabidhi Tuzo za Gawio Day 2025, Mchechu alipongeza mafanikio ya NMB kwa kukuza gawio lake kwa Serikali kwa asilimia 300 kutoka Sh. Bilioni 16 hadi kufikia Sh. Bil. 68.1, siri ya mafanikio hayo akiitaja kuwa ni ufanisi na ubora kiutendaji wa taasisi hiyo chini ya Afisa Mtendaji mzawa.
“Mheshimiwa Rais, Ofisi ya Msajili na Serikali tunajivunia sana ubora wa kiutendaji walioonesha Maafisa Watendaji Wakuu Wazawa, hususani Ruth Zaipuna wa NMB, wamethibitisha kwa vitendo kwamba hawajapewa nafasi hizo kwa kigezo cha uzawa wao, bali ubora na ufanisi wao kiutendaji.
“Kwa mfano NMB, imekuza gawio lake kwa Serikali kwa asilimia 300, kutoka Sh. Bil. 16.5 (mwaka 2014) hadi Sh. Bil. 68.1 na kwa hiyo Mheshimiwa Rais, hivi punde unaenda kupokea gawio la Sh. Bil. 68.1 kutoka NMB, wakati kuna baadhi ya taasisi na biashara ambazo, pato lao la jumla, haliwezi kufikia gawio la NMB kwa Serikali,” alisema Mchechu.
Katika Hafla hiyo, NMB ilipokea tuzo mbili kutoka kwa Rais Samia, ambaye alisema Serikali yake inatambua na kuthamini mchango wa Sekta Binafsi na taasisi ambazo zina hisa za Serikali, huku akizitaka kuimarisha Matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), ili kukuza pato lao na gawio la Serikali.
Rais Samia aliongeza kuwa, Gawio Day inaakisi dhamira thabiti ya kuhakikisha uwekezaji wa umma unaendelea kuleta matokeo chanya na wenye tija katika maendeleo ya kisera na kiuchumi ya taifa na kielezo cha juhudi, uwajibikaji na uadilifu wa Taifa katika kusimamia raslimali za umma na mrejesho wa mageuzi na maboresho.
NMB yakabidhi Gawio la Bil. 68.1/- kwa Serikali, Msajili Hazina aipongeza
Reviewed by Fahadi Msuya
on
June 10, 2025
Rating:
Post a Comment