CHUO CHA CATC CHAFAULU TATHMINI ILIYOFANYWA NA ICAO
Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC) kimekuwa miongoni mwa vyuo vilivyomo kwenye mtandao wa vyuo vya mafunzo ya usalama wa usafiri wa anga vipatavyo 35 duniani kote baada ya kufaulu tathimini iliyofanywa na Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO) mapema mwezi July 2022.
Akizungumza wakati wa kukabidhiwa Cheti pamoja na Bendera ya ICAO Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA) Hamza S. Johari amesema mchakato wa tathimini ya chuo cha usafiri wa anga umeanza mwezi Aprili na kumalizika mwezi July 2022 ambapo chuo hicho kimefaulu vigezo vya kuwa chuo cha mafunzo ya Usalama wa Usafiri wa anga cha kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika (ESAF).
Amesema kuwa hatua hiyo inafanya Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania kuwa miongoni mwa vyuo 6 vilivyoidhinishwa na kupata Ithibati ya ICAO kwaajili ya kutoa mafunzo ya usalama wa usafiri wa anga kwenye ukanda huu wa Afrika Mashariki, Kusini na Magharibi (ESAF/ WACAF) ambapo vyuo vingine vipo Dakar - Senegal, Douala - Cameroon, Johannesburg - Afrika ya Kusini, Lagos - Nigeria, Nairobi - Kenya.
"Mafanikio ya kuthibitishwa na kupata Ithibati hii kwa chuo chetu na kuwa miongoni mwa vyuo vya kikanda vya kutoa mafunzo ya usalama wa anga kunaenda sambamba na ongezeko la idadi ya wakufunzi watakaotoa mafunzo.
Hadi sasa, Tanzania ina wakufunzi 21 waliothibitishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (Certified National Aviation Security Instructors) Aidha, wapo wakufunzi wengine 9 ambao wamethibitishwa na ICAO (ICAO Aviation Security Certified Instructors) na wote ni Watanzania." alisema Johari
Pia amesema kuwa hatua hii ya uthibitisho (Certification) inakifanya chuo hicho kuwa na hadhi ya kutoa mafunzo kimataifa kwenye eneo la usalama wa usafiri wa anga.
Hii ni fursa ambayo italeta washiriki wa mafunzo hayo kutoka nchi mbali mbali duniani kulingana na mpango wa mafunzo wa chuo sambamba na mpango wa mafunzo utakaotolewa na shirika la usafiri wa anga Duniani yaani ICAO.
CHUO CHA CATC CHAFAULU TATHMINI ILIYOFANYWA NA ICAO
Reviewed by Fahadi Msuya
on
September 04, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
September 04, 2022
Rating:




Post a Comment