Header AD

header ads

Dkt. Ackson alitaka BMT kuongeza hamasa kwenye michezo ya Wanawake.



Na John Mapepele


Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe,  Dkt. Tulia Ackson amelitaka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuongeza hamasa kwenye michezo ya wanawake ili wanawake wengi zaidi washiriki kwenye michezo.

Akizungumza wakati wa kufunga tamasha la kimataifa la pili la michezo kwa wanawake   jijini Dar es Salaam leo, Oktoba 22, ameviomba  Vyombo vya Habari kuitangaza michezo  ya wanawake  ili  kuwe na hamasa kubwa kama ilivyo kwenye michezo ya wanaume. 


Ameipongeza Wizara na Baraza la Michezo la Taifa kwa kutekeleza majukumu yake ya kisheria kwa vitendo ambapo amesisitiza kuwa mafanikio makubwa ya Tamasha hili ni kielelezo tosha cha juhudi zinazochukuliwa katika kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika michezo na kutambua mchango mkubwa wa wanawake katika maendeleo ya michezo hapa nchini.

 "Ndugu Wanamichezo, Niipongeze Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Baraza la Michezo la Taifa kwa kuyatekeleza maelekezo ya Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha Tamasha hili mwaka jana. Ndani ya mwaka mmoja Tamasha hili limeendelea kukua na sasa limekuwa la kimataifa kwa kushirikisha wanamichezo kutoka Tanzania bara, Zanzibar, Kenya, Uganda na Zambia". Ameongeza Mhe. Spika


Aidha, amempongeza Mheshimiwa Rais kwa  kuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha na kuelekeza juu ya ushiriki wa Watanzania hususan wanawake katika michezo. 

“Mafanikio ambayo tunayaona kwa sasa katika sekta ya michezo ni matokeo ya juhudi kubwa zinazofanywa na Mheshimiwa Rais. Mathalan, sote tumeshuhudia Timu yetu ya Mpira wa Miguu ya Wanawake chini ya umri wa miaka 17 (Serengeti Girls), inayoshiriki kwa mara kwanza Mashindano ya Kombe la Dunia, inavyoendelea kuchanja mbuga ambapo imetinga hatua ya robo fainali.” Amefafanua Mhe. Ackson


Kwa upande wake  Katibu Mkuu wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Dkt, Hassan Abbasi amesema dhamira ya Serikali  kwa sasa  ni kulifanya  tamasha hilo kuwa la kimataifa kwa kushirkisha nchi kutoka mabara yote.

"Ndugu zangu waandishi napenda kusema kuwa kwa sasa tumejipanga, msije mkashangaa mwakani  katika tamasha la tatu nchi kama marekani kuja kushiriki tamasha hili”. Ameongeza Dkt. Abbasi


Kuhusu mpambano wa Simba na Yanga  hapo kesho amefafanua kuwa  kazi ya wizara ni kutoa  furaha kwa watanzania  hivyo amewasihi mashabiki kukubali matokeo  ya mchezo huo na kuendelea na  furaha kwani mchezo  wa soka ni furaha, upendo na umoja.


Dkt. Ackson alitaka BMT kuongeza hamasa kwenye michezo ya Wanawake. Dkt. Ackson alitaka BMT kuongeza hamasa kwenye michezo ya Wanawake. Reviewed by Fahadi Msuya on October 22, 2022 Rating: 5