MHE. MCHENGERWA AIPONGEZA TEMBO WARRIORS KWA KUIBAMIZA UZBEKISTAN 2-0
Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Mohamed Mchengerwa ameipongeza Timu ya Soka ya Taifa ya wenye ulemavu ( Tembo Warriors) kwa kuikandamiza Uzbekistan 2-0 kwenye mashindano ya kombe la Dunia ulemavu leo Oktoba 3, 2022 na kushika nafasi ya pili katika mundi lake nyuma ya Poland.
Akizungumza kwa baada ya ushindi huo, Waziri Mchengerwa amesema Serikali ya Tanzania ipo pamoja na timu hiyo katika kila hatua na ndio maana Rais ameridhia kuzigharimia timu hiyo kwa kila kitu ili iendelee kufanya vizuri.
“Rais na Serikali yenu ipo pamoja na nyinyi, endeleeni kulipigania Taifa lenu, onesheni uzalendo na kuhakikisha mnarudi na kombe nchini na hiyo itakuwa ni zawadi kwa Rais wenu mpendwa na watanzania wote kwa ujumla ”’ amefafanua Mhe. Mchengerwa.
Aidha ameendelea kusisitiza kuwa ahadi zawadi nono kwa timu hiyo ikiwemo shilingi milioni 40 endapo watafuzu robo fainali, shilingi milioni 80 wakifuzu kucheza nusu fainali na shilingi milioni 100 wakifanikiwa kufuzu fainali za michuano hiyo ipo palepale.
Amewataka wachezaji kuendelea kuzingatia nidhamu, umoja na kumtanguliza Mungu na kusema kuwa Serikali ipo kuhakikisha kila kitu kinakwenda vizuri.
Ameongeza kuwa akiwa nchini Uturuki anatarajia kufanya mazungumzo na Waziri wa Michezo na kusaini mkataba wa mashirikiano baina ya Tanzania na Uturuki katika sekta za michezo ili kusaidia kukuza sekta hiyo nchini Tanzania.
Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Hassan Abbasi alitoa wito Kwa wachezaji kujitokeza kwa wingi leo kushangilia timu ishinde ambapo wamejitokeza na kutoa hamasa kubwa.
Kwa upande wake Nahodha wa timu hiyo Steven Manumbu ameahidi ushindi kwa Mhe. Waziri na kusema kuwa timu ipo tayari kwa ajili ya kuipambania nchi yao.
MHE. MCHENGERWA AIPONGEZA TEMBO WARRIORS KWA KUIBAMIZA UZBEKISTAN 2-0
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 03, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 03, 2022
Rating:




Post a Comment