MILA NA TAMADUNI ZACHANGIA WATOTO WA TANGA KUINGIA KWENYE UKATILI
Na Hadija Bagasha Tanga,
Imebainika kuwa watoto wengi katika Mkoa Tanga wamekuwa wakiingia kwenye ukatili wa kijinsia kutokana na mila na tamaduni ikiwemo ngoma za asili jambo ambalo limekuwa likipoteza ndoto za vijana na watoto wengi pamoja na kuchangia kwa kiasi kikubwa mmomonyoko wa maadili kwa kundi hilo.
Mila na tamaduni zilizotajwa ni ngoma za asili pamoja na mila za baadhi ya makabila kuwachezea mabinti zao.
Baadhi ya wazazi wa eneo la Kismatui kata ya Pongwe jijini Tanga wametoa kilio chao wakati shirika lisilokuwa la kiserikali linalojihusisha na masuala ya kupiga vita aina zote za ukatili dhidi ya watoto na vijana balehe katika jiji la Tanga (TAYOTA) wakati lilipokutana na wazazi na wafunzi wa shule ya msingi Kismatui kwa lengo la kupingana na vitendo hivyo.
Halima Lupora ni mmoja wa wazazi katika eneo hilo amesema kuwa ngoma zao zinachangia kwa kiasi kikubwa kuwaharibu watoto wao hivyo wameomba elimu izidi kutolewa kila wakati ili wapunguze ukatili wa kijinsia na ngono zembe.
"Ngoma zetu za kiutamaduni na za kimila zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa sana kuwaharibu watoto wetu mwishowe wanajikuta wakiingia kwenye ukatili wa kijinsia sababu mtoto anapojua kwamba amechezwa anataka na yeye aende, "alisema Lupora.
Mzazi mwingine Mamtunda Shaban amesema baadhi ya wazazi wanachangia kwa kiwango kikubwa kuwaharibu watoto wao huku wakisahau ngoma wazowacheza watoto ndio zimekuwa zikiwaingiza kwenye vitendo vya ukatili.
"Ngoma za asili ni nzuri na ni mbaya kwanza tumezikuta enzi za mababu zetu lakini kubwa sana ni sisi wazazi ndio tunaowaharibu watoto wetu kama mimi mzazi mwanangu wa kike namcheza ngoma halafu akitoka pale kwenye ngoma na ni wanafunzi hatuwaruhusu kulala mapema tunawaacha waende kwenye vigodoro anarudi usiku wa manane au asubuhi jambo hili ni tatizo kubwa sana, "alisema Mamtunda.
Afisa Ustawi wa jamii kutoka Halmashauri ya jiji la Tanga Sella Mbughi amebainisha chimbuko la vitendo vya ukatili kuwa ni pamoja na familia nyingi kuwa mbali na watoto wao kutokana na majukumu na shughuli za kila siku.
"Kwa mimi ninavyoona chimbuko la hivi vitendo ni familia nyingi ziko bize na maisha mengine haziko bize kuwaangalia watoto mama yuko bize kwenye vigodoro baba yuko bize kwenye kutafuta kwahiyo wakirudi wamechoka watoto wakirudi kutoka shule hawajui wameshindaje huko walikotoka kwahiyo ishu ya malezi bado ni changamoto, "alisema Mbughi.
Mwalimu mkuu wa shule ya Msingi Kismatui Bakari Kobelo amesema kuwa wamekuwa wakikutana na kesi nyingi za vitendo vya ukatili ambapo mara baada ya kufuatilia wamegundua watoto wengi wameanzia majumbani vitendo hivyo.
kwa upande wake Afisa hamasa kutoka shirika hilo la Tayota ambaye pia ni balozi wa vijana Mkoa Tanga Seleman Msey amesema wanahakikisha wanafanya kazi ambayo Rais Samia anataka ya kulifanya Taifa kuwa Taifa lenye watu wenye huruma.
"Sisi tuko hapa Tayota kwa ufadhili wa Botner foundation kuhakikisha tunafanya kazi ambayo Rais wetu anataka katika kuhakikishaTaifa linakuwa na watu wenye huruma na linalolea, "alisistiza Msey.
Jackline Nambai ambaye ni msaidizi wa masuala ya kisheria amesema wameamua kutembea kwenye jamii na mashuleni ili kuibua vitendo vya ukatili
"Kuna matukio mengi ambayo watoto na vijana wanafanyiwa ukatili lakini ni matukio ambayo hayafiki sehemu yeyote na yanakuwa hayafiki sehemu yeyote na hayafanyiwi kazi kwahiyo tumeona tutembee kwenye jamii na, mashuleni kuibua vitendo hivyo, "alibainisha Nambai.
Ili kukomesha vitendo vya ukatili jamii pia imeaswa kutoa taarifa pindi wanapokutana na vitendo hivyo katika maeneo yao ili kuweza kuokoa jamii ambayo inakumbana na matukio ya aina hiyo.
MILA NA TAMADUNI ZACHANGIA WATOTO WA TANGA KUINGIA KWENYE UKATILI
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 18, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 18, 2022
Rating:






Post a Comment