Waziri Mchengerwa - Tamasha la Muziki wa Dansi laja
Na John Mapepele.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo. Mhe, Mohamed Mchengerwa amesema Serikali inakwenda kufufua muziki wa dansi uliokuwa umeanza kufifia kwa kuratibu tamasha kubwa la muziki wa dansi Novemba mwaka huu.
Mhe. Mchengerwa ameyasema haya wakati anamkaribisha Makamu Mwenyekiti wa CCM Taifa, Komredi Abdurahaman Kinana kwenye usiku wa Tamasha la Muziki la Grand Gala Dance kwa ajili ya kumbukizi ya miaka 23 ya kifo cha hayati Mwalimu Nyerere leo Oktoba 14, 2022 jijini Dar es Salaam.
"Ndugu Mgeni Rasmi, kama Taifa kuna kila sababu ya kurejesha utamaduni huu wa muziki hasa Muziki wa Dansi ambao umeanza kupotea katika kizazi cha leo. Kama nilivyoahidi mara baada ya kuteuliwa kusimamia Wizara hii kuwa Milango yangu ya Ofisi ipo wazi, Ninawakaribisha wadau wote wenye maono, mawazo ya jinsi ya kuurejeshea thamani thamani yake muziki wetu wa asili muziki wa dansi, ninawakaribisha sana. Wizara itashirikiana nanyi wakati wote na tumekuwa tukifanya hivyo, tutawasikiliza na kuwaunga mkono kila mwenye wazo ambalo linatuunganisha pamoja na kuturejesha kwenye fikra za Mwalimu." Amesisitiza Mhe, Mchengerwa
Ameongeza kuwa muziki wa dansi una mchango mkubwa kwenye uhuru wa nchi yetu na ukombozi wa bara la Afrika kwa ujumla hivyo kuna umuhimu wa kuufufua.
Mhe. Mchengerwa ameeleza kuwa kutokana na mchango wa Sanaa na Utamaduni, Serikali imeanzisha Mfuko wa Sanaa utakaowasaidia wasanii ili waweze kutumia kuboresha kazi zao.
Aidha, amemshukuru Rais, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu na kuzipa kipaumbele sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo (sekta za kimkakati) ambazo kimsingi ndio chimbuko la Utamaduni.
Amesema mataifa yote duniani yanatambuliwa na kutofautishwa na utamaduni wa taifa husika na katika karne hii ya Utandawazi mataifa mengi yanajitanabaisha kwa kutumia Muziki wake.
Amesema kwa kutambua hilo tayari Wizara imeshafanya jitihada za kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na mdundo wake wakiasili utakaotutambulisha duniani kote kama ilivyo kwa mataifa ya Jirani, Afrika ya kusini na kwengineko.
Tamasha hilo limeendeshwa na mshereheshaji nguli nchini Masudi Masudi huku mwimbaji maarufu na mtunzi wa wimbo wa Tanzania yetu ndiyo nchi ya furaha, Steven Hiza, Mhe. Nape na bendi mbalimbali kutumbuiza.
Waziri Mchengerwa - Tamasha la Muziki wa Dansi laja
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 15, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 15, 2022
Rating:




Post a Comment