WADAU WA MAKUMBUSHO WAMUENZI MWL. NYERERE KWA MSAFARA WA MAGARI YA ZAMANI
Na Mwandishi Wetu
Makumbusho ya Taifa kwa kushirikiana na wadau wa magari ya zamani (Oldschool ride Tanzania) wamemuenzi Mwl. J.K. Nyerere kupitia msafara wa magari ya zamani yaliyozunguka katika mitaa ya jiji la Dar es Salaam.
Msafara huo maalum wa magari ya zamani uliongozwa na gari la jeshi la polisi na kuleta shauku kwa watu wa jiji la Dar es Salaam ambao waliyashangaa na kushangilia magari hayo yaliyotengenezwa miaka ya 1930.
Msafara wa magari hayo aina mbalimbali ulianzia Mlimani City, ukapita Mwenge na Kuingia Kijiji cha Makumbusho ambapo wadau walipewa historia ya Mwl. Nyerere ambaye ni muasisi wa Kijiji hicho cha Makumbusho kilizoanzishwa mwaka 1967.
Aidha, waliweza kutembelea nyumba ya Kaya ya Wazanaki kabila analotokea Mwl. Nyerere. Wakiwa kwenye nyumba hiyo waliweza kuona vyakula vya asili vya kabila hilo na kucheza bao mchezo aliopendelea Mwl. Nyerere.
Msafara huo uliwashangaza watalii mbalimbali waliotembelea Kijijini hapo wakiwemo wazungu kutoka nchi ya Kanada ambao walifurahia msafara huo pamoja na ngoma zilizokuwa zinachezwa.
Baada ya hapo msafara uliendelea kuelekea mjini ambapo uliishia Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni palipohifadhiwa magari ya kihistoria aliyoyatumia Mwl. J.K. Nyerere wakati wa uhai wake.
Mkurugenzi wa Taasisi ya Magari ya Zamani, Bw. George Msambule amesema wameamua kuungana na Makumbusho ya Taifa kumuenzi Mwl. Nyerere kwa njia ya msafara wa magari ya zamani.
“Uhifadhi wa magari haya ni njia mojawapo ya kumuenzi Mwl. Nyerere muasisi wa Taifa hili, yanatoa elimu na ajira kwa vijana, amesema Bw. Msambule
Mratibu wa Mpango wa Miaka Kumi wa Kuenzi na Kutangaza Urithi wa Mwl Nyerere aliwapongeza wadau wa magari ya zamani kwa kuamua kujitoa kumuenzi mwl. Nyerere kwa njia ya magari hayo.
Amesema matukio mbalimbali yamefanyika katika kumuenzi Mwl.Nyerere ikiwa ni pamoja na maadhimisho ya Miaka 100 ya Mwl. Nyerere, mbio za baiskeli, Mbio za hiari za Mwl Nyerere Marathon na makongano mbalimbali.
Amewaalika wadau mbalimbali kushirikiana na Makumbusho ya Taifa katika kumuenzi Mwl. J. K. Nyerere.
WADAU WA MAKUMBUSHO WAMUENZI MWL. NYERERE KWA MSAFARA WA MAGARI YA ZAMANI
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 14, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 14, 2022
Rating:

Post a Comment