Header AD

header ads

DCEA YAKAMATA KILO 34.89 ZA HEROIN NA KUWASHIKILIA WATUHUMIWA 11 AKIWEMO KOCHA WA MAKIPA SIMBA




Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Vyombo vingine vya ulinzi na usalama kupitia operesheni waliyoifanya maeneo mbalimbali nchini wamekamata jumla ya kilo 34.89 za dawa za kulevya aina ya heroin na kukamata biskuti 50 zilizotengenezwa kwa kutumia dawa ya kulevya aina ya bangi ambapo jumla ya Watuhumiwa 11 walikamatwa na wanaendelea kuhojiwa.

Taarifa ya Mamlaka ya dawa za kulevya imewataja Watuhumiwa tisa (09) na kazi zao ambapo waliokamatwa kwa kukutwa na Heroin ni pamoja na Kocha wa Makipa Simba SC. ambaye pia ni Mchezaji wa zamani wa Simba Muharami Said Mohamedi (40). 


Kusaya aliwataja wanaoshikiliwa kwa tuhuma hizo ni Kocha wa Makipa wa Simba Muharam Said Sultani(40) mkazi wa Kigamboni na kufafanua kwamba Muharam amewahi pia kuichezea timu ya Simba.

Wengine ni Mfanyabiashara na Mmiliki wa Kituo cha Soka cha Kambiasso Sports Academy kilichopo Tuangoma wilayani Kigamboni Alhaj Kambi Zeber Seif maarufu kwa jina la Kambiasso au Alhaj Kambi.Alhaj Kambi mbali ya kumiliki kituo hicho cha soka ana miliki kampuni ya Safia Group of Companies inayomiliki magari ya kusafirisha abiria (daladala) kutoka Dar es Salaam kwenda Mkoa wa Pwani.

Pia Mamlaka hiyo inamshikilia Said Abeid Matwiko ambaye anaishi Magole A Kivule na kazi yake ni fundi selemala,mwingine ni Maulid Mohamed Mzungu maarufu kwa jina la Mbonde (54) mkazi wa Kisevule ambaye kazi yake ni mkulima.

Aliwataja watuhumiwa wengine ni John Andrew John (40) mkazi wa Magore-Kitunda ambaye ni mfanyabiashara na amekuwa na jukumu la kutafuta vijana wenye vipaji na kuwapeleka kituo cha Soka Kambiasso .Pia wanamshikilia Seleman Matola Said(24) mkazi wa Temeke –Wailes .Matola ni mtoto wa dada yake na mtuhumiwa Alhaj Kambi.

Mwingine ni Hussein Mohamed Pazi(41) mkazi wa Kibugumo wilayani Kigamboni ambaye ni mfanyabiashara na mtuhumiwa wa tisa ni Ramadhan Rashid Chalamila(27)ambaye ni mfanyabiashara. “Watuhumiwa wote wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani wakati wowote kuanzia sasa.”

Katika tukio lingine, Kamishina Jenerali Kusaya amesema Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya inamshikilia mtuhumiwa Abdulnasir Haruon Kombo(30) mfanyabiashara  na mkazi wa Ksloleni jijini Arusha akiwa na biskuti 50 zinazotengenezwa kwa kutumia dawa za kulevya aina ya bangi kama moja ya malighafi akiwa anaziuza katika eneo la Kaloleni.

“Aidha kuhusiana na tukio hili la ukamataji wa biskuti zenye bangi , tumefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mwingine anayeitwa Hassan Ismail(25) mkazi wa Olasiti jijini Arusha.”amesema.
 Kamishina Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Gerald Kusaya.
DCEA YAKAMATA KILO 34.89 ZA HEROIN NA KUWASHIKILIA WATUHUMIWA 11 AKIWEMO KOCHA WA MAKIPA SIMBA DCEA YAKAMATA KILO 34.89 ZA HEROIN NA KUWASHIKILIA WATUHUMIWA 11 AKIWEMO KOCHA WA MAKIPA SIMBA Reviewed by Fahadi Msuya on November 15, 2022 Rating: 5