UPATIKANAJI WA MAJI DAR SASA MAMBO SAFI, DAWASA YAFUNGUKA
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imefanikiwa kuongeza uzalishaji wa maji kwa Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani kutoka uzalishaji wa lita milioni 520 kwa siku hadi kufikia lita milioni 590 kwa siku.
Mafanikio haya ni matokeo ya juhudi kubwa zilizofanywa na Serikali kukamilisha utekelezaji wa mradi wa maji Kigamboni na kuongeza uzalishaji wa lita milioni 70.
Haya yameelezwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa DAWASA Mhandisi Cyprian Luhemeja kwenye mkutano na waandishi wa habari na kusema kuwa uzalishaji huu unaiwezesha Mamlaka kuweza kutoa huduma kwa wakazi wote wa Dar es Salaam na Pwani.
"Kupitia uzalishaji huu, naweza kusema kwa majimbo yote 16 ya uchaguzi ndani ya Dar es Salaam na Pwani yote yanapata huduma ya maji ya kutosha," amesema Mhandisi Luhemeja.
Ameongeza kuwa katika majimbo 10 ya uchaguzi yaliyopo Dar es Salaam likiwemo jimbo la Ilala, Kawe, Ubungo, Kibamba, Temeke, Segerea na Ukonga huduma ya maji inapatikana vzr.
"Kwa Kigamboni, kwa sasa huduma ya maji ipo ya kutosha kupitia mradi wa visima virefu ambavyo kwa sasa vinazalisha lita milioni 70, ambapo ifikapo Disemba Kigamboni itakuwa na lita milioni 98 za maji," amebainisha.
Kwa majimbo 6 ya uchaguzi ya Mkoa wa Pwani yakiwemo Bagamoyo, Chalinze, Mkuranga, Kibaha mjini na vijijini hali ya upatikanaji wa maji iko vizuri, kazi inaendelea ya kusogeza huduma ya maji kwa wananchi wa Chalinze baada ya kukamilika kwa mradi mkubwa wa maji wa Mlandizi - Chalinze - Mboga.
Pia kupitia utekelezaji wa mradi wa Chalinze awamu ya tatu, wakazi wa Kibaha vijijini wanatarajiwa kupata huduma kwa mwezi wa 12 mradi utakapokamilika. "Mpango tulionao DAWASA ni kuongeza uzalishaji wa maji kwenye Mtambo wa Ruvu Juu ambapo tutaongeza pampu moja kwa lengo la kufikia uzalishaji wa lita milioni 360 kutoka lita milioni 196 za sasa," amesema.
UPATIKANAJI WA MAJI DAR SASA MAMBO SAFI, DAWASA YAFUNGUKA
Reviewed by Fahadi Msuya
on
November 29, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
November 29, 2022
Rating:

Post a Comment