Header AD

header ads

HALI YA UPATIKANAJI WA UMEME NCHINI YAANZA KUIMARIKA



Na Yusuph Digossi

Shirika la umeme Tanzania TANESCO limesema kuwa iwapo mvua zitaendelea kunyesha katika mabwawa yote ya kufua umeme na matengenezo ya mitambo yaliyobakia kukamilika kama yalivyopangwa , hali ya umeme itaendelea kuimarika hivyo inatarajiwa kiasi cha upungufu wa umeme kwa siku kuendelea kupungua kutoka wastani wa kati ya megawati 300 hadi 350 wiki iliyopita hadi kufikia megawati 215 za umeme wiki hii.

Hayo yamebainishwa  na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO wakati akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa umeme nchini na jitihada zilizofanyika kukabiliana na hali ya upungufu wa umeme leo Ijumaa Desemba 02, 2022 katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwalimu Nyerere Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na waandishi wa  habari kuhusu jitihada za muda mfupi zilizokamilika  mkurugenzi mtendaji huyo amesema kuwa shirika hilo tayari tayari limeshakamilisha matengenezo ya mtambo mmoja wa LM600 katika kituo cha ubungo namba III huku akieleza kuwa mtambo huo umeshaanza kuingiza megawati 35 za umeme katika Gridi ya Taifa kuanzia 25 Novemba 2022 kama ambavyo TANESCO ilieleza hapo awali. 

"Tayari tumeshakamilisha matengenezo ya mtambo mmoja wa kituo cha Kidatu na umeshaanza kuzalisha megawati 50 za umeme katika Gridi ya Taifa kuanzia tarehe 30 Novemba 2022" amesema

Ameongeza kuwa “matengenezo ya mtambo mmoja katika kituo cha Kinyerezi namba II yameshakamilika na tayari umeshaanza kuzalisha megawati 215 za umeme kuanzia tarehe 24 Novemba 2022”

Kuhusu jitihada za muda mfupi zinazoendelea kufanyika Maharage amesema kuwa majaribio ya mitambo miwili katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi namba I yanaendelea, na kwa sasa mitambo hii inaingiza jumla ya megawati 65 za umeme katika Gridi ya Taifa.

“Tunategemea hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Disemba 2022, mitambo hii itakuwa inazalisha jumla ya megawati 90 kama tulivyoeleza hapo awali” amesema 

Aidha amesema  mitambo mingine miwili inatarajiwa  kuanza kufanya kazi katika kituo cha upanuzi cha Kinyerezi namba I kuanzia mwezi Februari 2023 ili kuingiza megawati 90 za umeme katika Gridi ya Taifa.
HALI YA UPATIKANAJI WA UMEME NCHINI YAANZA KUIMARIKA HALI YA UPATIKANAJI WA UMEME NCHINI YAANZA KUIMARIKA Reviewed by Fahadi Msuya on December 02, 2022 Rating: 5