Header AD

header ads

Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki haki za binadamu


Dar es Salaam. Serikali imesema inaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayo wawezesha wananchi kuendelea kunufaika na uhuru wa kutoa maoni ikiwa ni pamoja na haki ya kutoa na kupata taarifa.

Hayo yamesemwa Disemba 8, 2022 na Mkurugenzi wa haki za binadamu Wizara ya Katiba na Sheria, Ngasory Sarakikya wakati alipokuwa akizungumza katika maadhimisho ya siku ya haki za binadamu yaliyofanyika katika Ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Mwl. Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, akiwa ni mwakilishi wa Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro.

 “Serikali inaendelea kuweka mazingira rafiki ili wananchi waendelee na kunufaika na uhuru wa kutoa maoni na haki ya kutoa na kupata taarifa,” amesema Ngasory Sarakikya.

Ameongezea kuwa, Haki za kisiasa na demokrasia nchini zimekuwa zikiimarika kutokana na Serikali kukutana na kufanya majadiliano ya vyama vyote vya siasa na wadau mbalimbali. Huku haki nyingine zilizoripitwa kuimarika ni pamoja na haki za kiuchumi, kiraia, elimu na kupata huduma za kijamii ikiwemo maji.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Wakili Anna Henga amezitaja changamoto kadhaa zinazorudisha nyuma haki za binadamu nchini Tanzania ikiwemo haki ya kuishi ambayo imekuwa ikivunjwa kutokana na mauaji ya watu yanayoendelea nchini.
“Bado kuna changamoto mbalimbali, kwa mfano haki ya kuishi, haki ya kuwa huru na salama vinaendelea kuwa changamoto,” amesema Wakili Henga.

Pia ameyataja matukio mengine yaliyotokea ikiwemo mauaji yanayofanywa na vikundi vya uhalifu kama panya road, Mauaji baina ya wana ndoa yanayosababishwa na mume au mke pamoja na watu kujiua.
“Kuanzia Januari mpaka Disemba mwaka 2022 matukio 37 ya mauaji ya wenza yaliripotiwa, sababu kubwa ikiwa wivu wa mapenzi,” Amesema Wakili Henga.

Naye Katibu Mtendaji wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Patient Ntwina, amesema richa ya haki za binadamu kuendelea kuimarikani ni vyema Serikali kuchukua hatua juu ya changamoto zinazorudisha nyuma jitihada hizo kwani kila binadamu ana haki ya kuishi.
“Binadamu wote tunastahili kutendewa haki, kwa utu na kwa heshima na sisi sote tulizaliwa sawa na tunapaswa kutendewa kwa usawa,” amesema Ntwina.

Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki haki za binadamu Serikali kuendelea kuweka mazingira rafiki haki za binadamu Reviewed by Fahadi Msuya on December 09, 2022 Rating: 5