WATAALAMU KUENDELEA KUFANYA UTAFITI WA CHANJO YA EBOLA
Na Hadija Bagasha Tanga,
Wataalamu wa afya wamesema wanaendelea kufanya utafiti wa chanjo ya ugonjwa wa Ebola mpaka pale nchi itakapojiridhisha ubora na usalama wake kwa matumizi ya wananchi na ndipo itakapofanya maamuzi.
Kauli hiyo imetolewa na mratibu wa mafunzo ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii John Yuda kwenye mkutano wa tathimini ya programu na wadau 'RCCE' ya utoaji wa elimu ya afya kwa umma na ushirikishaji wa jamii katika majanga ya magonjwa ya mlipuko ulioshirikisha waratibu wa afya ya jamii kutoka Mikoa 11 iliyo katika hatari zaidi ya Ebola.
Mratibu huyo amesema kuwa wanaifuatilia kwa karibu chanjo ya ugonjwa wa Ebola ambapo wataalamu wapo kazini kuifanyia utafiti wa karibu chanjo hiyo pale patakapokuwa na uhitaji wa chanjo hiyo.
"Ni lazima kwanza tujiridhishe kwamba hii chanjo ni salama kwa wananchi wetu hakafu ndipo tutafanya maamuzi wakati huo ambapo umefika hivyo kama nchi na wataalamu tunafuatilia utafiti unaoendelea juu ya chanjo hiyo inayotengenezwa na nyingine tayari imeshafikia hatua ya kufanyiwa utafiti hivo tunasubiria, "alisisisitiza Yuda.
Aidha amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika mikusanyiko ya watu wengi pamoja na kuzingatia ushauri wa wataalamu katika kuzuia milipuko ya magonjwa mbalimbali na kuiasa jamii kujenga tabia ya kuosha mikono kila wakati.
Sambamba na hayo ameitaka jamii inayoishi maeneo ya mipakani ikatoa taarifa pale inapokuwa na mtu au mgeni aliyetoka, kwenye maeneo yaliyothibitika, kwamba yalitolewa taarifa kwamba kuna mlipuko wa ugonjwa huo.
"Jamii zinashirikiana kwa karibu ni vizuri zikatoa taarifa ili wataalamu waendelee kufuatilia wageni waliokuja, tuangalie afya zao jinsi zinavyokwenda kama kwa bahati mbaya ikionekana anao tuweze kuzuia nchi yetu isijeikapata mlipuko huu, "alisisitiza Yuda.
Kengia James ni mratibu wa tafiti na machapisho kutoka ofisi ya Rais Tamisemi idara ya afya amesema kuwa wanafanya mikakati mbalimbali ili kuweza kujikinga na magonjwa ya mlipuko na kuwataka wananchi wanaoishi maeneo ya mipakani kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali kutokana na taratibu ambazo imekuwa ikitoa kila mara.
"Kila maelekezo yanayotolewa na serikali ni muhimu kuyafuata cha msingi katika kupitia kamati za uelimishaji katika jamii na ushirikishwaji wa jamii katika udhibit wa magonjwa ya mlipuko hivyo kila kinachoelimishwa kupitia vyombo vya habari na taasisi za kidini kufuata ili kuweza kujikinga, "alisema
Kwa upande wake Katibu wa afya mwandamizi idara ya afya ofisi ya Rais Tamisemi Chipole Mpelembe amesema kuwa malengo ya kikao hicho ni kutaka kila mkoa ujifunze kutoka kwa mkoa mwingine ikiwa ni pamoja na kupeana uzoefu na mafanikio katika mwaka uliopita wa utekelezaji wa kazi mbalimbali kwa wadau wa maendeleo.
"Kikao hiki ni cha wadau wa maendeleo ambao wanafanya kazi kwenye eneo la utoaji wa elimu ya afya kwa umma katika jamii zetu kuhusu magonjwa ya mlipuko mbalimbali ikiwemo kimeta, kipindupindu, leptospirosis na sasa Ebola, "alibainisha Mpelembe.
Kikao hicho kitakaa kimeshirikisha waratibu wa elimu ya afya ya jamii na maafisa afya wa Mikoa 11 yenye hatari zaidi ya kupata maambukizi ya ugonjwa wa Ebola kwa siku tatu mfulilulizo lengo likiwa ni kuimarisha afua za utoaji wa elimu ya afya kwa umma na ushirikishwaji wa jamii.
Mikoa iliyoshiriki kikao hicho ni pamoja na Mikoa ya Kanda ya Ziwa kwamaana ya Mwanza, Geita, Mara, Kagera, Kigoma, Arusha, Kilimanjaro, Daresalaam, Mbeya na Songwe, pamoja na waratibu kutoka Mkoa wa Ruvuma.
WATAALAMU KUENDELEA KUFANYA UTAFITI WA CHANJO YA EBOLA
Reviewed by Fahadi Msuya
on
December 14, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
December 14, 2022
Rating:







Post a Comment