Header AD

header ads

Waziri Kairuki atoa maagizo yanayogusa viongozi, watumishi




NA OR-TAMISEMI

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Angellah Kairuki ametaka viongozi kuongeza kasi katika uchukuaji wa hatua dhidi ya wale wote wanaokwenda kinyume na taratibu za utumishi wa umma.

Waziri Kairuki ameyasema hayo leo Februari 28,2023 wizarani jijini Dodoma wakati akizungumza kwenye kikao cha Menejiment cha mapokezi ya viongozi wapya wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI.


Amesema,katika kusimamia mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa kuna changamoto za kiutumishi ambazo zinatokea, lakini viongozi wamekuwa wagumu kuchukua hatua stahiki kwa watumishi hao, hivyo kuanzia sasa kiongozi ahakikishe anachukua hatua stahiki za kinidhamu katika maeneo ambayo yanaweza kuleta taswira hasi kwa Serikali.

Aidha, amewataka viongozo wote kuacha kufanya kazi kwa mazoea,kwani kunazorotesha jitihada za Serikali za kuwaletea wananchi maendeleo.

Pia amesisitiza kufuatilia na kufanya tathmini (Performance Tracking) ya utendaji kazi wa watumishi na kuona matokeo ya wale ambao wanawasimamia ili kama sehemu kunalega au kuna mabadiliko hatua zichukuliwe.


"Mtumishi anaweza kuwa vizuri na mchapa kazi kwa wakati fulani,lakini baada ya muda unakuta amebadilika utendaji kazi wake unazorota, sasa hapo ndipo mnapotakiwa kufuatilia na kufahamu mabadiliko hayo yametokana na nini na kumuwezesha kuendelea na majukumu kikamilifu,"amesisitiza Waziri Kairuki.

Pia amewataka viongozi hao kushauriana na kushirikishana katika utendaji kazi wao ili kuleta uelewa wa pamoja katika kuwahudumia wananchi jukumu ambalo limenabeba taswira nzima ya Wizara ya OR-TAMISEMI.


Mhe. Kairuki amewataka viongozi hao kusimamia ujibuji wa hoja za Ukaguzi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa  ili kuhakikisha kuwa zinapungua au kufungwa kabisa na sio kuziacha hoja  hizo ziendee na kusababisha dosari kwa Serikali kila wakati.

Wakati huo huo Mhe. Kairuki amesisitiza usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa  katika Mamlaka za Serikali za Mitaa ili thamani ya fedha ionekane na iweze kuwezesha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

"Fedha nyingi  zimepelekwa  kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza miradi ya Elimu, Afya pamoja na Miundombinu simamieni kuhakikisha miradi hiyo inakamilika na inatoa huduma na kama kuna miradi chechefu muisimamie ikamilike pia,"amesisitiza Waziri Kairuki.

"Hakikisheni mnafuatilia matumizi ya fedha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kama fedha imeelekezwa ikajenge madarasa ikafanye kazi hiyo na si vinginevyo," amesema Waziri Kairuki.

Amewataka pia viongozi hao kusimamia masuala mtambuka ya Lishe na Udumavu kwa kuzingatia mkataba wa lishe aliosaini Mhe. Rais na Wakuu wa Mikoa yote nchini hivyo taarifa ya kila wakati inatakiwa kuona maendeleo katika eneo hilo.

Kwa upande wake Naibu Waziri Mhe. Deogratius Ndejembi amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa kumuamini na kuendelea  kumpa nafasi ya kuwatumikia wananchi na kusema yupo tayari kushirikiana na  watumishi wote wa Ofisi ya Rais TAMISEMI ili kwa pamoja kuwahudumia wananchi.
Waziri Kairuki atoa maagizo yanayogusa viongozi, watumishi Waziri Kairuki atoa maagizo yanayogusa viongozi, watumishi Reviewed by Fahadi Msuya on February 28, 2023 Rating: 5