Matapeli 11 wa mitandao ya simu waswekwa rumande Tanga

Na Hadija Bagasha Tanga,
Jeshi la polisi Mkoa wa Tanga linawashikilia watu 11 waliokuwa wameweka kambi jijini Tanga na kuendesha wizi kwa njia ya mtandao katika Mikoa mbalimbali nchini ikiwemo ya Kanda ya Kaskazini.
Watuhumiwa hao 11 wanaohusishwa na utapeli kwa njia ya mtandao wamekuwa wakituma ujumbe mfupi wa maneno na namba za simu kwa watu mbalimbali wa kuomba kutumiwa pesa.
Akithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao Kamanda wa Polisi Mkoa Tanga Henry Mwaibambe ameeleza kuwa aina ya utapeli waliobainika kuutumia watuhumiwa hao baada ya kuwahoji wamesema kuwa walikuwa wakimtaka mwenye simu kutuma fedha na wengine kuomba namba za siri.
Kamanda Mwaibambe amesema watuhumiwa hao walikuwa wamepanga nyumba katika eneo la Donge jijini Tanga na kulipa kodi ya mwezi mmoja na kulipia shilingi laki nane ili waweze kukamilisha utapeli wao wamekutwa na simu,line za simu 42 ,jiko na chotezo kwa ajili ya kuchomea line na karatasi zenye orodha za namba walizokwishatapeli na wanazotarajia kuendesha utapeli huo pamoja na fedha shilingi za Tanzania,Dola za Marekani na fedha za Congo DRC.
Watuhumiwa hao walikutwa pia na kadi za simu za mitandao mbalimbali, pikipiki, kadi za benki 5, simu ndogo za tochi 13 za aina mbalimbali, simu 11 kubwa za smartphone.
Fedha za kitanzania walizokutwa nazo ni shilingi milioni mbili na elfu themanini na tano, fedha za Congo DRC shilingi 45,100 na dola moja ya kimarekani.
"Tulichokibaini sisi polisi ni kwamba Karatasi tulizowakuta nazo zilikuwa na orodha ya majina ya watu ambao waliotapeliwa walikuwa wakiwekewa alama ya tiki na ambao wapo kwenye mchakato wa kutapeliwa wakiwekewa alama ya H huku waliotapeliwa mara mbili wakiwekewa alama za tiki 2,"
Aliongeza kuwa tuliwakuta na vocha 2 za shilingi elfu moja moja za mtandao wa Airtel , katarasi 43 zilizoandikwa namba za simu na namba za mawakala kwa majina mbalimbali ya watumiaji wa namba hizo vitambulisho mbalimbali 14, betri za simu ndogo 7, chaji za simu 7 za aina mbalimbali. Alisema Kamanda Mwaibambe.
Kamanda Mwaibambe amewataja waliokamatwa na kuhusishwa na utapeli huo kuwa ni Hadija Nyange (34) mkazi wa Muheza,Zaina Athumani (25) mkazi wa Mwanzange,Innocent Omeme (35) wa Dar es salaam,Abdulaziz Nzori (31) wa Dar es salaam, Said Hassan (24) wa Dar es salaam, Rashid Habibu (23) wa Dar es salaam,Said Juma (30) ,Idd Kaniki (35),David Rupiana wa Dar es salaam (22),Omary Mohamed (27) wa Mkanyageni Tanga na Salum Rajab (24) wa Dar es salaam.
"Hawa watu ni watu hatari sana tusiposhirikiana na jeshi la polisi hatuwezi kuwafunga na mtu asione aibu kutoa taarifa pindi anapotapeliwa hii itasaidia kukomesha matapeli hawa, "alisitiza Kamanda Mwaibambe.
Matapeli 11 wa mitandao ya simu waswekwa rumande Tanga
Reviewed by Fahadi Msuya
on
July 20, 2023
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
July 20, 2023
Rating:

Post a Comment