MWENYEKITI CCM TANGA AHOJI KUCHELEWA KWA ZAHANATI YA MATEMBONI
Na Hadija Bagasha Tanga,
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga Rajab Abrahaman Abdalah amehoji sababu za kuchelewa kwa mradi wa zahanati ya kijiji cha matemboni kilichopo kata ya Maramba Wilayani Mkinga Mkoani Tanga ambayo ilianza ujenzi toka mwaka 2013 ambapo mpaka sasa bado haijakamilika.
Mwenyekiti Rajab alibaini matumizi mabaya ya fedha kwenye zahanati hiyo ya ambayo hadi sasa tayari imetumia kiasi cha shilingi milioni 62 huku wakibakisha milioni 3 ambazo haziwezi kumaliza ujenzi huo ambao hadi sasa wanajenga zahanati hiyo kwa miaka kumi sasa.
Kufuatia hatua hiyo Mwenyekiti Rajab amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mkinga Kanal Maulid Sulumbu kufuatilia kwa karibu matumizi sahihi ya fedha zilizotumika katika ujenzi wa mradi huo na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliohusika kula fedha za serikali.
Mwenyekiti Rajab ameyasema hayo wakati alipofika kituoni hapo mara baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo ambapo ameonyesha kukerwa na usimamizi mbovu wa matumizi ya fedha za serikali uliofanyika kwenye mradi huo.
Mwenyekiti Rajab alisema ilani ya CCM inaelekeza kila kijiji kiwe na zahanati lakini viongozi hao kwa miaka kumi wameshindwa kuwaondolea wananchi kero ilidumu miaka mingi na kusababisha akina mama wajawazito kujifungulia njiani wakifuata huduma Vijiji vya jirani.
"Niwasihi viongozi wote kwamba kila aliyepewa dhamana na serikali lazima atimize wajibu wake msipofanya haya mnakifanya Chama Cha Mapinduzi kipate wakati mgumu inapofika uchaguzi wakati fedha zinaletwa lakini viongozi wanashindwa kuzisimamia, kiukweli chama hakijaridhika na kimesikitishwa na uzembe wa viongozi kushindwa kusimamia fedha hizi," alisema Mwenyekiti.
Mbunge wa jimbo hilo Dastani Kitandula amekiri kweli kuchelewa kwa mradi huo ambao umechukua muda mrefu kumalizika kutokana na changamoto mbalimbali.
"Tulipokuja na kamati ya mfuko wa jimbo kuja kukagua zahanati hii tukagundua kwamba kuna nyufa nyingi tukaagiza wajenzi wa wilaya waje kukagua kwamba jengo hili linaweza kuendelea au tulibomoe mainjinia walikuja wakafanya tathimini yao wakasema jengo linaweza kufanyiwa ukarabati likaendelea na Halmashauri ikapewa jukumu hilo la kumalizia zahanati hii wwenzetu wakajipanga fedha zikatolewa lakini tangu kazi hiyo imeanza sikupata bahati ya kutembelea, "alisema Kitandula.
Mbunge wa jimbo hilo Dastan Kitandula alimpa Mwenyekiti huyo salamu za Rais Dkt Samia kwamba wameridhika na kazi anazozifanya hasa kuwaletea fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali wilayani humo.
Baadhi ya wananchi katika eneo hilo wamesema kuchelewa kwa mradi huo kunawasababishia shida kubwa wakinamama wajawazito ambao wanakosa mahali pa kujifungulia huku wengine wakijifungulia majumbani na njiani wakienda kufuata huduma hiyo.
Wananchi hao wamemuomba Mwenyekiti Rajab kuweka msukumo katika suala ujenzi wa zahanati hiyo ili kuweza kuokoa maisha ya watanzania.
MWENYEKITI CCM TANGA AHOJI KUCHELEWA KWA ZAHANATI YA MATEMBONI
Reviewed by Fahadi Msuya
on
July 31, 2023
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
July 31, 2023
Rating:




Post a Comment