Tasnia ya Chai yafanya mapinduzi makubwa Saba Saba
NA MWANDISHI WETU
TASNIA ya Chai Tanzania, ilijidhatiti kutoa elimu na huduma mbalimbali kuhusiana na zao na bidhaa ya chai kwa wananchi waliotembelea banda lao katika Maonesho ya Biashara ya Kimataifa ya Mwalimu J.K. Nyerere, yanayoisha hivi punde jijini Dar es Salaam.
Banda la tasnia hiyo inayoundwa na Bodi ya Chai Tanzania (TBT) na Wakala wa Maendeleo ya Wakulima Wadogo wa Chai Tanzania (TSHTDA), linapatikana ndani ya jengo la Katavi lililopo eneo la Wizara ya Kilimo, mtaa wa kwanza kushoto kama unaingia geti kuu la viwanja vya Saba Saba.
Akizungumza na wanahabari katika banda lao, Ofisa Mipango wa (TSHTDA), Mtalemwa Samwel, alisema kuwa wameshiriki katika maonesho hayo ili kuitangaza tasnia yao na shughuli zao wanazozifanya viweze kujulikana nchi nzima na duniani kwa ujumla.
“Tupo katika maonesho haya ili kuitangaza tasnia na washirika wake na shughuli zetu tunazozifanya ambazo ni kukuza na kujenga uwezo wa wakulima wadogo wa chai, kuwezesha utoaji wa huduma za ugani kwa wakulima wadogo wa chai, kujenga na kuimarisha umoja wa wakulima wadogo wa chai kupitia vikundi na vyama vyao pamoja na kuwezesha uendeshaji wa kilimo cha chai katika maeneo mapya.“Pia tunawahamasisha wakulima wadogo wa chai kujenga na kuendesha viwanda vyao kwa ajili ya kusindika majani yo mabichi ya chai ili waweze kushiriki katika mnyororo wa thamani ya zao hilo kuanzia shambani, kuchakata hadi sokoni,” alisema.
Kwa upande wake, Ofisa Mipango Mkuu na Uhamasishaji wa TBT, Godlove Myinga, alisema kuwa pamoja na mambo mengine, wamejitosa kwenye maonesho hayo ili kujitangaza wao na fursa zilizopo katika mnyororo wa thamani ya chai na kuielimisha jamii juu ya faida za kiafya ya kutumia zao hilo.
“Tunashukuru tumepata mwitikio mkubwa kwa wananchi kutembelea banda letu la chai na tumekuwa tukiwaelimisha chai ni nini na fursa zilizopo katika sekta ya chai.
Pia tumekuwa tukiwapa elimu juu ya imani potofu kuwa chai ina sumu kwa kuwapa maelezo kwamba ni kinywaji kizuri na ni kama dawa ya mitishamba inayosaidia kuondoa magonjwa mbalimbali.
“Chai ina madini ya manganese na zinki inayosaidia mmeng’enyo wa chakula mwilini na pia madini ya phosphorus yanayosaidia kusisimua misuli na kuondoa mafuta yaliyomo katika damu, hivyo tumekuwa tukiwatangazia wananchi kuwa chai si sumu na kwamba wanaweza kuitumia muda wowote wanaojisikia,” alisema Myinga.
Aliwataka wananchi wanaotembelea maonesho ya Saba Saba kutembelea banda lao ili kupata maelezo juu ya majukumu ya Tasnia ya Chai Tanzania (TBT na TSHTDA) na kufahamu faida za kunywa chai, bidhaa na huduma zao mbalimbali pamoja na kuonjeshwa chai ya bure.
Mmoja wa wananchi waliotembelea banda hilo, Mariam Saleh, alisema kuwa amefarijika mno kutokana na elimu aliyopewa na maofisa wa banda la tasnia hiyo ya chai, hasa faida za kunywa chai, lakini pia aina mbalimbali za kinywaji hicho.
“Kilichonifurahisha zaidi, pamoja na kuelimishwa juu ya faida za kunywa chai na kilimo cha zao la chai kwa ujumla, tumepewa chai ya bure. Nawashauri watanzania wanaokuja kwenye maonesho haya ya Saba Saba wasiache kufika katika banda hili la Tasnia ya Chai Tanzania,” alisema Mariam.
Tasnia ya Chai yafanya mapinduzi makubwa Saba Saba
Reviewed by Fahadi Msuya
on
July 14, 2023
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
July 14, 2023
Rating:

Post a Comment