WAZIRI JAFO ASHIRIKI ZOEZI LA USAFI MWISHO WA MWEZI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akishiriki katika zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi katika Soko la Bonanza jijini Dodoma pamoja na wafanyabiashara katika soko hilo leo Julai 30, 2022 na kusisitiza agenda ya usafi wa mazingira kuwa endelevu.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akisukuma mkokoteni uliobeba taka kuelekea katika vyombo maalumu vya kuhifadhi taka kabla ya kusafirishwa kwenda Dampo mara baada ya kushiriki katika zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi katika Soko la Bonanza jijini Dodoma pamoja na wafanyabiashara katika soko hilo leo Julai 30, 2022
Waziri wa Nchi ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo akizungumza na wafanyabiashara katika Soko la Bonanza jijini Dodoma mara baada ya kukamilika kwa zoezi la usafi katika soko hilo leo tarehe 30/07/2022.
*******************************************
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Selemani Jafo leo Julai 30,2022 ameshiriki katika zoezi la usafi wa mwisho wa mwezi katika Soko la Bonanza Jijini Dodoma.
Akiwa sokoni hapo amezungumza na wafanyabiashara na kutoa rai kwao kudumisha kwa vitendo kampeni ya usafi na mazingira kwa ujumla.
“Ndugu zangu agenda ya mazingira ni endelevu sote yatupasa kuitekeleza kwa vitendo na uwe ni utamaduni wetu sote” Dkt. Jafo alisisitiza.
Pia, amewapongeza wafanyabiashara sokoni hapo, mabalozi wa mazingira na wananchi kwa ujumla kwa kujitokeza kushiriki kufanya usafi wa mazingira.
Amemwelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) ndani ya kipindi cha siku 14 kuhakikisha anafanya ukarabati wa mfumo wa maji taka katika soko hilo ili kuondoa adha inayowakumba wafanyabiashara kwa sasa.
“Ukarabati huu wa Mfumo wa maji taka katika eneo hili ufanyike mara moja, Mkurugenzi wa DUWASA asimamie kwa karibu utekelezaji wake” Alisisitiza Dkt. Jafo.
Aidha, Waziri Jafo alisema kuwa Serikali inatarajia kuzindua Kampeni ya usafi wa mazingira itakayofahamika kama ‘My Dustbin’ kwenye mitaa ya mbalimbali nchi nzima.
Alisema kampeni hiyo itasaidia kuweka mitaa katika hali ya usafi kwa kuwa kila mwananchi anatakiwa kutupa taka kwenye mapipa yaliyoyopo kwenye mitaa badala ya kutupa ovyo.
Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Mazingira na Udhibiti wa Taka ngumu wa Jiji la Dodoma Bw. Dickson Kimaro alisema wamekuwa wakihamasisha wananchi kushiriki usafi wa mazingira ili kuweka jiji katika hali ya usafi. Bw Kimaro alilisitiza uwajibikaji wa kila mwananchi katika kuhakikisha usafi unafanyika Mita tano kuzunguka maeneo ya Makazi na Biashara.
Alisema katika soko hilo wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla wamekuwa wakijitokeza kushiriki katika kufanya usafi wa mazingira sokoni hapo hivyo kuliweka jiji katika hali ya usafi.
WAZIRI JAFO ASHIRIKI ZOEZI LA USAFI MWISHO WA MWEZI
Reviewed by Fahadi Msuya
on
July 30, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
July 30, 2022
Rating:




Post a Comment