WIZARA NA JESHI WAUNDA MIKAKATI YA KUBORESHA MICHEZO KIMATAIFA.
Na John Mapepele
Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania wameweka mikakati kabambe ya kushinda kwenye mashindano ya michezo yanayokuja hivi sasa ili kuendelea kuitangaza Tanzania kimataifa.
Katika kikao cha pamoja baina ya Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo, Saidi Yakubu na ujumbe wa Kurugenzi ya Michezo kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania mbali ya kuweka mikakati ya muda mfupi na muda mrefu wamekubaliana kuanzisha vituo vya kulea vipaji vya michezo (Sports Academy) nchini ili kuzalisha vipaji vya wanamichezo watakaoweza kufanya vizuri.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Kaimu Katibu Mkuu, Bwana Saidi Yakubu amesema kuwa ni ukweli usiopingika kuwa majeshi yana hazina kubwa ya vipaji vya michezo ambavyo kama vikitumika vizuri vitasaidia kuipeleka nchi katika kiwango cha kimataifa kwenye michezo.
Ameitaja baadhi ya mikakati iliyojadiliwa kuwa ni pamoja na kuwa mpango wa maandalizi wa kushiriki kwenye mashindano ya Olympiki na Mashindano ya Afrika, kuendeleza miundombinu ya michezo, kuwa na mashirikiano ya Sports Academy na kuingia makubaliano ya kisheria(MoU) kwenye michezo baina ya Jeshi na Wizara.
Ameelekeza kufanyika kikao kujuadili masuala ya kiufundi ndani ya muda usiopungua siku saba baina ya Wizara na Jeshi ili kuja na mpango wa utekelezaji wa muda mfupi na mrefu ili utekelezaji wake uanze mara moja.
Aidha amesema kikao hicho cha kujadili mambo ya kiufundi pia kitajadili namna bora ya kuwashirikisha wadau mbalimbali wa michezo ili kuleta tija katika mikakati hiyo.
Mkurugenzi wa Michezo wa Jeshi la Wananchi Tanzania Kanali Martin Sterwart amemshukuru Kaimu Katibu Mkuu Yakubu kwa mwongozo alioutoa ambapo amemhakikishia kwa upande wa jeshi watakwenda kutekeleza mara moja kwa faida ya taifa zima.
WIZARA NA JESHI WAUNDA MIKAKATI YA KUBORESHA MICHEZO KIMATAIFA.
Reviewed by Fahadi Msuya
on
September 13, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
September 13, 2022
Rating:



Post a Comment