Mhe. Mchengerwa atimiza ahadi ya kuwapa Tembo Warriors donge nono, awapongeza Simba kwa ushindi, awatakia heri Serengeti Girls.
Na John Mapepele
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Mohamed Mchengerwa ametimiza ahadi ya Serikali ya kuwazawadia donge nono Timu ya Soka ya Taifa ya Tembo Warriors iliyoshiriki mashindano ya Kombe la Dunia kwa watu wenye ulemavu nchini Uturuki na kushika nafasi ya saba kidunia aliyoahidi wakati timu hiyo inakwenda kwenye mashindano hayo hivi karibuni.
Akiongea leo, Oktoba 11, 2022 jijini Dar es Salaam kwenye hafla ya kuikaribisha nyumbani na kuipongeza timu hiyo, amesema mafanikio ya ushindi huo unatokana na utashi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan katika kuwekeza kwenye michezo na hamasa ya watanzania kwenye michezo kwa ujumla.
Aidha, amefafanua kwamba ushiriki wa Tembo Warriors katika mashindano haya umesaidia kuitangaza Tanzania duniani na amewataka wanamichezo wengine wanaoshiriki mashindano ya kimataifa kuiga mfano wa Tembo Warriors kuweka uzalendo mbele na kupigania nchi yao.
Amewaagiza watendaji wa mashirikisho ya michezo nchini kushirikiana na Serikali kuvisaidia vilabu vinavyocheza mashindano ya kimataifa huku akiwataka watendaji wa Serikali kusimamia kikamilifu mashindano yote ya kimataifa ili kupata matokeo tarajiwa.
Amesisitiza kuwa kama vilabu vyote vya michezo vitaweka maslahi ya taifa mbele na kuacha kufikiria maslahi binafsi michezo itafika mbali.
Ametumia nafasi hiyo kuipongeza Timu ya Simba kwa kuishinda 3-1 timu ya C.D Primeiro de Agosto ya Angola katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na kuwatakia kila la kheri Timu ya Soka ya Taifa ya Serengeti Girls inayocheza kesho na Timu ya Taifa ya Japan katika mashindano ya Dunia chini ya umri wa miaka 17 yanayoanza kesho nchini India.
Amewataka Watendaji wa Wizara kuwakumbusha vilabu vyote kukamilisha mpango kazi wa kujenga miundombinu ya michezo kama walivyokubalina katika kikao cha hivi karibuni baina ya wizara na vilabu vyote vya michezo huku akisisitiza kuwa hiyo ni kulingana na matakwa ya sera ya michezo inayoelekeza kila klabu kuwa na miundombinu. Pia amewataka wadau kuwekeza katika michezo ili kuinua michezo.
Mhe. Waziri Mchengerwa ametoa rai kwa kila taasisi kuwa; Michezo kuwa sehemu ya vipaumbele vya Taifa katika Sera, mikakati na mipango mbalimbali ya maendeleo ya Kitaifa, ngazi mbalimbali za Serikali (Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Miji, Majiji na Mashirika ya Umma), kutenga fedha kwa ajili ya kugharamia shughuli za Michezo kila mwaka ili kuwezesha umma wa Tanzania kushiriki katika michezo; na kuendelea kuhamasisha wadau wa ndani na nje ya nchi kuchangia katika Sekta ya Michezo nchini ikiwa ni pamoja na kugharamia ushiriki wa timu za Taifa katika mashindano ya kimataifa.
Aidha, amesema michezo ni nyenzo muhimu ya kuleta mabadiliko katika jamii ikiwemo; kuelimisha jamii katika masuala ya afya, elimu, mapambano dhidi ya dawa za kulevya na utunzaji wa mazingira.
“Mchango wa sekta ya michezo katika maendeleo ya Taifa lolote ni mkubwa sana na unajidhihirisha katika nyanja mbalimbali ikiwemo katika kutoa ajira, kuongeza pato la Taifa; kulitangaza Taifa, kuimarisha umoja, undugu, uelewano, mshikamano na ushirikiano ndani na nje ya nchi”. Amesisitiza Mhe. Mchengerwa
Akitoa historia fupi ya timu hiyo katika mashindano hayo, Makamu wa Rais Athuman Lubandame amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kusaidia.
Mtendaji Mkuu wa Shirika la BIMA la Taifa (NIC) Dkt. Elirehema Doriye ameipongeza Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa kazi nzuri inayofanya chini ya Waziri Mchengerwa ya kuendeleza michezo. NIC ni miongoni mwa wafadhili wa Tembo Warriors ambao wametoa milioni 40 kama zawadi kwa timu hiyo kufuzu robo fainali.
Mhe. Mchengerwa atimiza ahadi ya kuwapa Tembo Warriors donge nono, awapongeza Simba kwa ushindi, awatakia heri Serengeti Girls.
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 11, 2022
Rating:
Reviewed by Fahadi Msuya
on
October 11, 2022
Rating:




Post a Comment